Kortini Akidaiwa Kusema Tanzania ina Wagonjwa 200 wa Corona
0
April 11, 2020
Moshi. Mfanyabiashara wa mjini Moshi, African Mlay (58), amefikishwa kortini akituhumiwa kuandika taarifa kwenye mtandao wa Jamiiforums kuwa Tanzania ina wagonjwa zaidi ya 200 wa Covid-19.
Hata hivyo, mfanyabiashara huyo aliyefikishwa mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi, Sophia Masati, aliachiwa kwa dhamana akiwa na wadhamini wawili waliosaini dhamana ya Sh10 milioni.
Wakili wa Serikali kutoka ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Kassim Nassir alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Machi 26, 2020 kwa kutuma maandishi hayo katika mtandao huo.
Kwa mujibu wa Kassim, alidai siku hiyo akiwa katika Manispaa ya Moshi, mshitakiwa alitumia simu yake ya mkononi kutuma ujumbe wa uongo katika kundi la Whatsapp lililopewa jina la Jamii Forums.
Maneno anayodaiwa kuyaandika yaliyopo katika hati ya mashitaka ni “Kwanini Serikali ya Tanzania inaficha sana takwimu za ugonjwa wa corona? Kumekuwa na usiri mkubwa mno wa ugonjwa huu wa corona”
Maneno hayo yanaendelea” Mpaka sasa Serikali imedai ina wagonjwa 12 tu na ambao wote wamepona. Kwa lugha nyingine Tanzania corona ni zero (sifuri) kwamba hakuna mgonjwa hata mmoja tena”.
“We are free from corona (hatuna tena corona) lakini ukweli sio huu wa Ummy Mwalimu (waziri wa afya) na Serikali ambao wanafanyia siasa afya za watu,”anadaiwa kuandika hivyo na kuendelea;-
“Ukweli uliopo mpaka sasa Tanzania kuna wagonjwa 200+ (zaidi ya 200) wa corona na mpaka sasa waliokufa na corona ni wagonjwa 4 na hii yote imefanywa siri ya serikali na idara zake za takwimu”
“Je! Inatusaidia nini kuwa na usiri mkali kwa janga la kitaifa? Wakina Paul Makonda wanazunguka kila kona kumshukuru Mungu kwa kuwa mtoto wa Mbowe (Freeman) kaambukizwa corona.”
“Hawa ndio wengi wao katika serikali ya nchi ya Tanzania,” anadaiwa kumalizia ujumbe wake hivyo, matamshi ambayo upande wa mashitaka unadai ni uongo na sio sahihi na yanalenga kupotosha jamii.
Akanusha shitaka hilo
Mshitakiwa alikana shitaka hilo wakati Wakili Kassim aliiambia mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na Hakimu Mkazi, Sophia Masati akapanga Aprili 15, 2020 kuwa ndio siku ya kusomwa kwa maelezo ya awali ya kesi hiyo.
Mwananchi
Tags