Licha ya Kutafuna Mil. 850, Gari la Mondi Lakwama Kuja Bongo




KWA wafuatiliaji wa mitandano ya burudani Bongo, mkoko mpya wa mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ aina ya Rolls Royce unaotajwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 850 za Kibongo siyo habari ngeni, IJUMAA WIKIENDA linakujuza habari mpya kuhusu gari hilo.

LILIANZIA MITANDAONI

Picha na video za gari hilo la kifahari vilianza kusambaa wiki iliyopita ambapo Diamond au Mondi aliliposti likiwa na jina lake (Platnumz) kwenye mtandao wake wa TIk TOk bila kuweka maelezo kama limeshatua Bongo au la.

Baadhi ya mashabiki wake walizichukua picha na video hizo na kuanza kusambaza kwenye kurasa mbalimbali za Instagram huku mashabiki wakitoa maoni tofauti.

WAPO WALIOPONGEZA

Kuna ambao walipongeza kwa kitendo cha yeye kununua gari hilo kwani umaarufu wake unakwenda kufanana na mafanikio yake kwani sasa anakwenda kutembelea gari linalotumiwa na mastaa mbalimbali wakubwa duniani hasa wale wa Marekani.

“Ni mwanzo mzuri, anadhihirisha kwamba kweli yeye ni Simba hapa Bongo na hakuna mwingine,” alichangia mdau mmoja kwenye ukurasa wa Globalpublishers wa Instagram.



WENGINE WAPONDA

Hata hivyo, Waswahili hawakukosea waliposema kwenye msafara wa mamba kenge huwa hawakosekani kwani mbali na watu wengi kusifia gari hilo, wapo waliokosoa.

Waliokosoa walikuwa na hoja mbalimbali, lakini kubwa waliyoishikia bango ni ile ya kwa nini mkali huyo wa Wimbo wa Jeje anashindwa kujenga nyumba na kuishia kununua vitu vya anasa kama gari hilo.

“Mtu ana kanyumba kamoja tu, tena anaishi mama yake sasa hivi, sasa kwa nini asijenge?” Alihoji Jesco Kitwe kwenye Instagram.

LAKWAMA KUJA BONGO

Kikizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, chanzo makini kilichopo ndani ya Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya Mondi, kilieleza kwamba, licha ya Mondi kufanikisha malipo ya gari hilo nchini Marekani, lakini limekwama kuingia Bongo kutokana na janga la maambukizi ya Virusi vya Corona.

“Jamaa ameshakamilisha kila kitu kule Marekani, lakini ishu ni kwamba sasa hivi kule hali ni mbaya, Corona imewazuia wafanyakazi kwenda makazini,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Ingekuwa si Corona, basi gari hilo lingeshatua Bongo tangu mwanzoni mwa mwezi huu (Aprili), lakini sasa ndiyo hivyo imeshindikana na haijulikani hali itakaa sawa lini kama unavyoona kila siku maambukizi yanaongezeka.”


MAREKANI HALI NI MBAYA

Hadi juzi Jumamosi iliyopita, Marekani ndiyo nchi inayoongoza kwa maambukizi ya Virusi vya Corona ambapo ilikuwa na maambukizi 710,272 na vifo vilikuwa 37,175.

Janga hilo limezuia shughuli mbalimbali za kiuchuni kwenye nchi karibu zote duniani ambapo kwa Tanzania, hadi juzi Jumamosi, tayari kuliripotiwa maambukizi 147 na vifo vitano vilivyotokana na ugonjwa unaosababishwa na Virusi vya Corona wa COVID -19.

MONDI ANASEMAJE?

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilijaribu kumvutia waya Mondi ili kumsikia anazungumziaje mkwamo huo wa gari lake, lakini simu yake iliita bila kupokelewa.



BABU TALE AFUNGUKA

Baada ya kumkosa Mondi, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilimtafuta mmoja wa mameneja wa msanii huyo, Hamisi Taletale ‘Babu Tale’ ambapo alipopatikana alikiri kwamba gari hilo limekwama kwa sababu ya maambukizi ya Virusi vya Corona.

“Sasa hivi hata kioo cha simu kikiharibika siyo rahisi kukipata madukani kwa sababu ya maambukizi ya Virusi vya Corona, sasa unafikiri hiyo gari inaweza ikaja kirahisi hivyo? Haiwezi kwa sababu ya Corona, tunasubiri hadi hali itakapokaa sawa,” alisema Tale.

NI GARI YA NDOTO YAKE

Inakumbukwa Mondi alishawahi kuhojiwa kwenye chombo kimoja cha habari na kueleza kuwa gari la ndoto yake ni Rolls Royce ambapo alisema kuwa, atalinunua mwaka 2016.

Hata hivyo, Mondi alishindwa kukamilisha ndoto yake hiyo hivyo endapo Corona itakapotoweka, basi msanii huyo anakwenda kuitimiza ndoto hiyo.

SIFA ZA GARI HILO

Ndani ya gari hilo la Mondi kuna siti zenye nafasi kubwa na zenye ubora wa hali ya juu ambapo katika siti wanazozitazama abiria wa nyuma, kuna skrini ndogo za kisasa zinazofunuka na kujifunika kwa kuongozwa na dereva au abiria aliyepanda.

Utulivu wa kwenye gari ni wa hali ya juu, kwani kwa namna lilivyoundwa si rahisi kusikia hata mashimo kirahisi hivyo kuwafanya abiria na dereva kuwa ‘comfortable’ wanapokuwa ndani hata kama litapita kwenye barabara yenye mashimo. Kama hiyo haitoshi, kuna kifriji kidogo katikati ya siti ya nyuma kwa ajili ya kupoozea vinywaji na eneo maalum la kuwekea glasi ambapo hata kuwe na mtikisiko si rahisi kudondoka.

MTAALAM WA MAGARI AFUNGUKA

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na mtaalam wa kuuza magari aitwaye Abdulatif Shabaan, mkazi wa Ilala jijini Dar ambaye anauza magari tofauti ya kifahari ambapo alilitaja gari kama hilo la Mondi kuwa moja kati ya magari ya kifahari duniani.

Alisema japo magari hayo yanatofautiana kwa maana ya muundo na mwaka yaliyotengenezwa, lakini bado aina hiyo ya gari ndiyo inayokamata usukani kwa kuwa na magari ya kifahari duniani. “Rolls Royce ndiyo aina ya magari yanayoongoza kwa magari ya kifahari duniani, sidhani kama hapa Bongo kuna mtu analo, kama lipo basi ni kwa kuhesabu sana ila Sauz (Afrika Kusini) nafahamu yapo.

“Unajua haya Rolls Royce yapo ya muundo tofautitofauti, kuna kama hilo la Mondi ambalo ni Rolls-Royce Sweptail, kuna Rolls Royce Phantom Black, Rolls Royce Wraith, Rolls Royce Dawn yaani kifupi yapo ya aina nyingi.

 

STORI: MEMORISE RICHARD NA KHADIJA BAKARI, DAR

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Dua ya KondeBoy...!!!
    Ya Dhuluma siku zote kwa Mungu hayapiti

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad