Magufuli asema Tanzania haitafunga mipaka, kuzuia watu ndani kwa sababu ya corona


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema Serikali haitafunga mipaka wala kuwazuia watu kutoka ndani ili kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona kwa sababu kufanya hivyo kutasababisha madhara ndani na nje ya Tanzania.

Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Aprili 10, 2020 katika Kanisa Katoliki Parokia ya Mlimani Wilaya ya Chato mkoani Geita alipoungana na waumini kusali ibada ya Ijumaa Kuu iliyoongozwa na Padri Innocent Sanga wa jimbo Kuu Katoliki la Mbeya.

Taarifa iliyotolewa na mkurugenzi wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inamnukuu kiongozi mkuu huyo wa nchi akisema Serikali ya Tanzania imeamua kutowazuia watu ndani ya nyumba zao wala kufunga mipaka kwa kutambua madhara makubwa yanayoweza kujitokeza kutokana na kufanya hivyo ndani ya nchi na kwa nchi nane ambazo zinategemea kupata huduma na bidhaa kupitia Tanzania hususani Bandari ya Dar es Salaam.

Amewataka Watanzania wote kuendelea kumuomba Mungu ili aiepushe dunia na janga la ugonjwa wa corona.

Amebainisha kutokana na madhara ya ugonjwa huo duniani, upo uwezekano wa kutokea upungufu wa chakula na kutoa wito kwa Watanzania kuzalisha chakula cha kutosha.

Amewataka Watanzania kuendelea kuchapa kazi kila mahali walipo huku wakichukua tahadhari za kutoambukizwa kama wanavyoelekezwa na wataalamu.

Mapema leo Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu alieleza hali ya ugonjwa huo akibainisha kuwa wagonjwa wamefikia 32, watano wamepona na waliofariki dunia wakifikia watatu.

Katika ibada hiyo, Magufuli alimshukuru padri huyo kwa mahubiri yaliyowakumbusha Wakristo kuwa msalaba unaokoa na kupitia msalaba Mungu ataiokoa dunia dhidi ya majanga mbalimbali ukiwamo ugonjwa wa corona.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad