MSEMAJI wa Simba, Haji Manara amefunguka kuwa Ugonjwa wa Covid-19 unaonezwa na Virusi vya Corona vimetibua dili lake la kuwaleta nchini Wazungu wa Klabu ya Olympique Lyonnais ambao walikuwa wanakuja kwa ajili ya kuangalia vipaji.
Manara amesema kwamba alipata dili na klabu hiyo baada ya kwenda nchini Ufaransa hivi karibuni na walikubali kuja Aprili 28, mwaka huu lakini virusi hivyo vimetibua kila kitu.
Virusi hivyo vimekuwa tishio duniani kutokana na kusambaa kwake kwa kasi na Ufaransa ni moja ya nchi ambazo zina maambukizi mengi.
Manara amesema: “Nia yangu kubwa kwenye safari zangu ni kwa sababu nina kampuni inayojihusisha na promosheni na nia yangu ni kuungana na mawakala wa soka kwa lengo la kuwachukua vijana wa Tanzania na kuwapeleka nchi mbalimbali za Ulaya.
“Baada ya kuwatafuta Wazungu hao wakaniambia kwamba hawatachukua wachezaji wakubwa wa Simba, Yanga au Coastal badala yake watachukua vijana chini ya miaka 16 au 17, walikuwa wanakuja Aprili 28 lakini Corona imezuia hilo.
“Ilikuwa niandae mashindano ya timu za Dar na nyingine ambazo zingekuja kushiriki ambapo Klabu ya Lyon wangewachukua lakini pia kuna timu nyingine nazo zilikuwa tayari kuwachukua vijana hao japokuwa walikuwa wanataka wakae chini yangu kwa muda kabla ya wao kuja kuwachukua.”