MATRONI wa Hospitali moja nchini Uingereza ambaye ameonekana katika picha ya pamoja na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Boris Johnson amefariki dunia kwa maambukizi ya virusi vya corona ‘Covid-19‘ ikiwa ni siku chache kabla ya kustaafu kazi yake hiyo.
Sara Trollope, 51, ambaye ni mama wa watoto wanne na bibi, amehudumia taifa hilo kwa miaka 33 katika Idara ya Afya kabla ya umauti kumkuta huko Watford General Hospital, Jumamosi iliyopita kufuatia kuugua covid-19 kwa wiki moja.
Trollope, alikuwa akifanya kazi kama mwangalizi wa wagonjwa wa akili ambao ni watu wazima katika Hospitali ya Hillingdon na alipiga picha hiyo akiwa na Waziri Mkuu Boris mwaka jana wakati kiongozi huyo alipotembelea hospitali hiyo jimboni kwake.
Rafiki wa Trollope aitwaye Chris Wilson anasema “ni jambo la kushangaza na ilikuwa zawadi ya pekee ya kibinadamu kutoka kwa Mungu.”
Kila mmoja amekuwa akimsifia kwa namna yake; “Alikuwa mwanamke shupavu na wa kushangaza, alitaka kuwa nesi. Sara amewasaidia sana wagonjwa na wafanyakazi wenzake, aliipenda sana kazi yake na kila mmoja alikuwa akimpenda. Lakini kwa masikitiko, kazi hii ndiyo imeondoa uhai wake.”
Trollope alikuwa akimhudumia pia mumewe, Gary ambaye alijeruhiwa akilitumikia taifa lake Jeshini na kushindwa kuendelea na kazi. Ameacha watoto wa kike wawili ambao ni Gemma na Freya na mapacha wa kiume ambao ni Kyle na Michael.
Trollope alifanya kazi kwa kujituma bila kuchoka, na alikuwa na morali ya kazi mara zote kwa wagonjwa na watu aliyowahudumia.
Zaidi ya wahudumu 30 wakiwemo madaktari na wauguzi katika Idara ya Afya nchini Uingereza wameshapoteza maisha mpaka sasa kwa covid 19 tangu ugonjwa huo uingie nchini humo. Jumla ya watu 85,212 wameshaambukizwa coronavirus na watu 10,612 wameshapoteza maisha Uingereza kutokana na janga hilo hatari duniani.
Johnson aliruhusiwa kutoka katika Chumba cha Wagonjwa Mahtuti (ICU) kwenye Hspitali ya St. Thomas jijini London jana Jumapili baada kukaa hukio kwa siku kadhaa kufuatia kuzidiwa na corona. Waziri Mkuu huyo atakaa chini ya Uangalizi kwa wiki kadhaa mpaka atakapopona kabibsa ndipo atarejea ofisni kuendelea na majukumu yake.