Dar es Salaam. Baada ya kuthibitika kuwa amepona ugonjwa wa corona, meneja wa mwanamuziki Diamond Platnumz, Sallam Sharaf ‘SK’ amefunguka kuhusu kuumwa kwake na jinsi alivyofanikiwa kupona.
Machi 19 kupitia ukurasa wake wa Instagram, meneja huyo alikuwa ametoka safari katika nchi za Ufaransa, Ubelgiji na Uswisi aliweka wazi kuwa ana virusi vya corona.
Akizungumza katika mahojiano na mtandao wa Dizzim Online jana, Sallam alieleza kuwa licha ya ukweli kuwa ugonjwa huo ni tishio, taarifa zisizo sahihi zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kuzua taharuki.
Sallam alisema pamoja na jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na wataalamu duniani kote kukabiliana na ugonjwa huo, taarifa ambazo zimekuwa zikitolewa ni zile zinazohusu vifo na watu mahututi huku ripoti za watu waliopona zikiwa hazipewi nafasi kubwa zaidi.
“Habari nyingi ni za kutisha na hata siku niliyotangaza kuwa nina ugonjwa wa corona ilikuwa ngumu mno kwangu maana ndugu zangu na watu wangu wa karibu wakawa wananipigia simu, wakilia na kuamini kama ningekufa. Hii ilinipa wakati mgumu hata mimi niliyekuwa naumwa,” alieleza Sallam.
Alipongeza jitihada zinazofanywa na Serikali kuwaangalia wagonjwa wa corona ikiwa ni pamoja na kuwapatia huduma bora na kuwafuatilia maendeleo yao kila kukicha kwenye vituo vya kutoa tiba hiyo.
Alianzaje kuumwa
“Nakumbuka ilikuwa Ijumaa ya Machi 13, nikiwa Ufaransa niliamka asubuhi mwili ukiwa unauma na nikawa najisikia homa.
“Nilianza kujihisi kwamba nina corona nikawaambia wote niliokuwa nao wakae mbali na mimi na wakaanza kuchukua tahadhari.
“Siku hiyo ndiyo tukapata taarifa ya kusitishwa matamasha yote ya muziki, tukaanza kutafuta usafiri wa kurudi Tanzania.
“Uwanja wa Ndege wa Paris ulikuwa umefungwa ikatubidi tuendeshe gari umbali wa saa nane hadi Zurich, Uswisi kwenda kutafuta usafiri wa kurudi Tanzania,” alisema Sallam, ambaye alikuwa Ulaya na mwanamuziki Diamond.
Alisema wakati wote wa safari alikuwa na homa kali na alikuwa akijituliza na dawa aina ya panadol ili aweze kupata nafuu lakini bado aliendelea kujisikia vibaya.
“Nilipofika uwanja wa ndege jijini Dar es Salaam nikatengeneza mazingira ya kujitenga. Nikachukua gari ya kukodi ya Uber, nilipofika nyumbani wafanyakazi wangu akiwamo mlinzi na dereva niliwaeleza wakae mbali na mimi, yote hiyo ni kutengeneza mazingira ya kukwepa kuwaambukiza.
“Nilikaa nyumbani kwa siku tatu nikiwa nafanya mawasiliano na madaktari nikiwaleza hali yangu, waliniambia kwanza nijipime joto likaonekana kali ndipo walipokuja kunifuata na gari la wagonjwa na kunipeleka kwenye kituo maalumu cha Temeke nikiwa mgonjwa wa mwanzoni kabisa,” alisema.
Maisha yake kituoni
Sallam alieleza kuwa kati ya watu watano waliokuwa wakihudumiwa katika eneo hilo la kutengwa, yeye ndiye alikuwa mwenye hali mbaya zaidi na hakutarajiwa kuondoka mapema kabla ya wenzake.
“Kiukweli mimi niliumwa sana wenzangu walikuwa na nafuu zaidi. Homa yangu ilikuwa inapanda zaidi hadi kufikia nyuzi joto 39.7, ilitengeneza taharuki kwa madaktari hadi kufikia hatua ya kuchukua damu na kuangalia vipimo vingine wakakuta kila kitu safi. Ilibidi waniweke dripu za dawa za antibiotic, paracetamol na glucose,” alisema Sallam.
Alisema pamoja na kuumwa, mwili wake ulikuwa na uchovu kutokana na kutopata muda mrefu wa kupumzika kutokana na shughuli zake.
Alisema kutobadilika kwa hali yake kuliwafanya madaktari wamuhoji kama anatumia dawa za kulevya, jambo ambalo amedai hajawahi kufanya.
“Ile hali ya homa kuwa juu madaktari wakanifuata na kutaka niwaambie ukweli kama natumia dawa za kulevya, nikawaambia kwamba sijawahi kutumia dawa wala kuvuta sigara. Hawakuridhika wakamuuliza hata dereva wangu.
Mtungi wa oksijeni
Sallam alieleza kuwa kufuatia hali yake kuwa mbaya na kuonekana akipata shida wakati wa kupumua, madaktari walifikia uamuzi wa kumuwekea hewa ya oksijeni.
“Usiku nilikuwa napumua kwa kuguna, kwangu hiyo ndiyo ilikuwa nafuu, wenyewe wakaona kwamba napata shida sasa siku hiyo asubuhi wakaniletea mtungi kwa ajili ya kuniwekea hewa ya oksijeni.
“Hapo ndipo nikashtuka nikaona hali inakoelekea si kuzuri ilibidi nianze kujipa nguvu na kujichangamsha ili nisiwekewe ule mtungi.
Nilikuwa natapika kila nikila, nikaanza kujikaza kula kwa kujilazimisha.
Baada ya hapo ikawa ni machungwa mfululizo, chai ya tangawizi na limao hadi hali yangu ilipokaa sawa na hatimaye kukutwa nimepona nikaruhusiwa,” alisema Sallam.
Source: Mwananchi