Nyepesi Nyepesi..Harmonize Atajwa Kumhujumu Ali Kiba


NYUMA ya pazia la muziki wa Bongo Fleva, kuna vita nyingi na kubwa za kimyakimya! Tukio la wasanii wawili wa Bongo Fleva, Killy na Cheed kutimka kwenye Lebo ya Kings Music inayomilikiwa na supastaa wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’, limeibua mapya.



HARMO ATAJWA

Kufuatia tukio hilo la mapema Jumanne wiki hii, madai mazito yameshushwa yakimtaja mkali mwingine wa Bongo Fleva, Rajab Abdul ‘Harmonize’ na lebo yake ya Konde Music Worlwide almaarufu kama Konde Gang, kuwa naye anahusishwa na ishu hiyo.

Madai mazito ya mtaani yanasema kuwa, awali kulianza manenomaneno ya chini kwa chini juu ya Killy na Cheed kuondoka kwa Kiba kwa madai tofautitofauti.

Hata hivyo, chanzo makini kimeeleza kwamba, kadiri muda ulivyokwenda, ndivyo chipukizi hao walivyokuwa wakipaza sauti kuwa wanataka kuondoka kwenye lebo hiyo.

SAUTI ZAMFIKIA MWANADADA

Inasemekana kwamba, sauti hizo zilimfikia mwanadada mmoja wa mjini ambaye awali alikuwa na ukaribu na Kiba, lakini kwa sasa yupo karibu na Harmonize au Harmo.

Inadaiwa kwamba, mwanadada huyo ambaye pia ana ukaribu na wasanii hao wa Kiba, alitumia ukaribu huo kuwashawishi kuondoka kwa Kiba huku Lebo ya Harmo ya Konde Gang ikitajwa kama kituo chao cha pili.

MUDA MFUPI BAADA YA KUSEPA

Ghafla tu, muda mfupi baada ya taarifa nyingi kusambaa kuwa wasanii hao wa Kiba wamesepa kwenye lebo hiyo, kulianza kuenea stori nyingine kuwa, chanzo cha wasanii hao kuondoka ni mwanadada huyo.

Madai hayo hayakuishia hapo kwani yalimtaja Harmo kuwa anahusishwa kumhujumu Kiba ambaye ana ugomvi wa kukata na shoka na mwanadada huyo ambaye ameahidi kumwaga siri za Kiba.

MOTO WAWAKA

Kufuatia kusambaa kwa ishu hiyo, ndipo moto ukawaka ile mbaya huku kila timu ya mtandaoni ikitumia lugha zisizokuwa na staha.

MENEJA AFUNGUKA

Baada ya kuinyaka ishu hiyo, gazeti hili liliwatafuta mameneja wa wasanii ambapo yule wa Kiba, Essi Mgimba, simu yake iliita bila kupokelewa huku yule wa Harmo, Beauty Mmary ‘Mjerumani’ akifunguka kila kitu anachokijua;

“Hakuna ukweli wowote na hatuwezi kuwasajili hao wasanii.

“Kuhusiana na hizo tetesi zinazosambaa kuwa sisi tunahitaji kuwasajili hao vijana, waache waseme wenyewe (wasanii) labda wanatamani kujiunga na Konde Gang.

“Hata hivyo, siyo kitu kibaya kama wanataka kujiunga, lakini sisi kwa sasa hatuna ubavu wa kusajili msanii yeyote mwingine.

“Hii ni kwa sababu tumeshasajili mmoja na ndiyo tupo tunaangalia je, yupo vizuri sokoni? Hivyo, kwa sasa nisiseme uongo, hatuwezi kusajili msanii mwingine yeyote.

“Pia hatutaki kuzungumzia wasanii wa Kiba kwa sababu sisi tunadili na wasanii wengi na hatukurupuki, tunaangalia na kipaji cha mtu kama kinaendana na sisi kwa sababu sisi tunafanya biashara,” alisema Beauty ambaye hana makuu.

KUONDOKA KWA WASANII WA KIBA

Taarifa za Killy na Cheed kujitoa Kings Music zilianza kusambaa Jumanne iliyopita baada ya wasanii hao wenyewe kuandika kwenye kurasa zao za mitandao yao ya kijamii ikiwemo Instagram, lakini hawakuweka wazi sababu za kujitoa kwao.

“Naitwa Ally Killy maarufu kama Killy, nilijulikana kama msanii wa Kings Music Records, napenda kuwajulisha fans (mashabiki) wangu wote waliokuwa waki-support (kuunga mkono) mziki wangu na wanaoendelea ku-support kazi zangu na hata wasioni-support pia kwamba kuanzia leo (Jumanne iliyopita) napenda kutamka kuwa mimi siyo msanii tena wa Kings Music.


“Nimeamua hili kwa akili yangu kabisa bila kushawishiwa na mtu yeyote wala sijatumia kilevi chochote. Hii ni kwa ajili ya mwendelezo wa muziki wangu.



“Ali Kiba amekuwa ni mtu muhimu sana kwenye maisha yangu, amenionesha njia na kuniaminisha mimi pamoja na muziki wangu mbele ya jamii, Inshaallah Mwenyezi Mungu amlipe kwa kila alichonifanyia na kujitolea kwa ajili ya muziki wangu, namshukuru sana na sitaacha kumshukuru na ninaumia sana ila sina budi. Nakupenda sana my brother,” aliandika Killy.

Kwa upande wake, msanii Cheed naye alitumia ukurasa wake wa Instagram kutangaza kung’atuka kwake kwenye lebo hiyo ambapo kama ilivyo kwa Killy, alieleza shukrani zake kwa Kiba huku akimuomba amuombee dua kwenye safari yake ya muziki.

UHUSIANO WA KIBA NA HARMO

Wakati Harmo anaondoka kwenye Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) iliyo chini ya Mwanamuziki Nasibu Abdul ‘Diamond’, zilisikika tetesi kuwa huwenda anakwenda Kings Music kwa Kiba.

Hata hivyo, baada ya Harmo kuanzisha lebo yake ya Konde Gang, tetesi hizo hazikusikika tena.

Baadaye yalisikika tena madai ya kwamba, hawako vizuri kufuatia kukutana kwenye msiba wa msanii Mbalamwezi ambapo hawakusalimiana na kuibua gumzo kubwa.

Kwa nyakati tofauti, Kiba na Harmo wamekuwa wakikanusha kuwa, hakuna jambo lolote baya kati yao.

STORI: MEMORISE RICHARD, RISASI

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad