RC Wangabo awataka wananchi kulinda mipaka huku 49 wakiwekwa karantini Mkoani Rukwa


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka viongozi wa vitongoji, vijiji pamoja na watendaji wao wa kata za Korongwe na Kabwe kuhakikisha wanawahamasisha wananchi katika maeneo yao kuwa mstari wa mbele katika kuilinda nchi kutokana na ugonjwa wa Corona kwa kuzuia uingiaji holela wa wageni wanaoweza kuuleta ugonjwa huo kutoka nchi za jirani.

Mh Wangabo amesema kuwa hadi sasa mkoa wa Rukwa umewaweka Karantini watu 49 ambapo kati ya hao watanzania 36 na wageni 13 ambao walipita katika bandari na mipaka rasmi ya mkoa huo na kusisitiza kuwa katika utekelezaji wa kuwaweka watu Karantini hauangalii uraia wa mtu wala hadhi yake, na kuongeza kuwa inachokijali serikali ni usalama wa wananchi wake dhidi ya ugonjwa hatari wa Corona.

Hivyo amewataka viongozi hao kuwaelimisha wananchi kuwakataa wageni wasiotumia mipaka na bandari rasmi kuingia katika nchi kwani kutofanya hivyo kutailetea nchi maafa makubwa na hivyo na hivyo kuwataka viongozi na wananchi kuacha matumizi ya bandari bubu zilizopo katika vijiji vya mwambao wa ziwa Tanganyika.

“Waende wakapite katika maeneo ambayo ni rasmi, waje hapa kwenye bandari ya Kabwe, wapite hapo na taratibu nyingine za kiafya zitafanyika, lakini sio kwenye bandari bubu huku, bandari bubu ni marufuku kutumika, ndani ya wilaya hii ya Nkasi kuna bandari bubu 46, Nkasi peke yake na katika kata zenu mbili hizi, ya Korongwe na Kabwe kuna bandari bubu 13, ndio maana nikasema viongozi ninyi wa kata mbili hizi mje hapa, ili muone umuhimu wa kuzuia watu kiholela holeal kuja kwenye bandari hizi bubu,” Alisisitiza.

Mh. Wangabo ameyasema hayo wakati wa kikao na wenyeviti wa vitongoji na vijiji vyenye bandari bubu pamoja na watendaji wa kata Kabwe na Korongwe zinazobeba vijiji hivyo katika kikao kilicholenga kutoa elimu ya ugonjwa wa Corona kwa viongozi hao pamoja na kutoa maelekezo ya serikali dhidi ya mapambano ya ugonjwa huo.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Rukwa Kamishna Msaidizi Elizeus Mushongi alitahadharisha matumizi mabaya ya madaraka ya viongozi hao ambao huwapokea wageni hao na kuwaruhusu kuingia katika nchi bila ya kufuata utaratibu wa serikali na kuongeza kuwa matumizi ya bandari bubu ni haram una hivyo atakayekamatwa anahalalisha matumizi ya bandari hizo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

“Wageni kutoka nje ya nchi, iwe Kongo, iwe Burundi, iwe Zambia, mnawapokea kule na nyinyi ndio mnakuwa maafisa uhamiaji, mnakuwa maafisa forodha, kila kitu mnamaliza wenyewe kule, sasa kama mtampokea mtu anaumwa ule ugonjwa, ninyi ndio mtakaoanza kuupokea ule ugonjwa kabla ya wote na bila ya kujua mtaenda kuambukiza familia na familia kama dokta alivyosema, niwaombe sana msipokee watu kutoka nje ya nchi kama hawajapita katika vituo vilivyoainishwa kisheria,” Alisema.

Aidha wakati akitoa salamu zake kwa mkuu wa mkoa, Diwani wa Viti Maalum Mh. Christina Simbakavu alisema kuwa kuna baadhi ya watu wenye ndugu zao nchi ya jirani ya Kongo huwa na kawaida ya kuingia katika vijiji hivyo nyakati za usiku na ndugu zao huwapokea katika utaratibu ambao unaweza kuhatarisha maisha yao.

“Kuna boti zinazoingia usiku kama alivyotamka mjumbe wa Kijiji cha Kalila, zile boti zinaingia lakini wenyeji wenye ndugu zao kutoka nchi jirani ya kongo wanawapokea katika mazingira ambayo sio Rafiki sana na hawatoi taarifa, na hili nalo linafukuta lakini hatujapata uhakika uliowazi, tunajaribu kuongea na wananchi kuwa tusipokee wageni wa aina yoyote na nawaomba viongozi wangu tuhamasishe utumiaji wa maji na sabuni kunawa na katika nyumba zetu tuweke vifaa hivyo,” alisema.

Naye Diwani wa Kata ya Korongwe Mh. Venus Bamilitwaye wakati akitoa neno la shukurani ka mkuu wa mkoa wa rukwa aliwasisitiza viongozi wa kata hizo kuhakikisha wanashirikiana na wananchi katika kulinda bandari bubu pamoja na kuzuia uingiaji wa kiholela wa wageni jambo ambalo ni hatari kwa afya ya wananchi wa mkoa wa Rukwa na Tanzania.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad