Sakata la Waafrika China Kufukuzwa Majumbani na Kulala Mitaa, China Yalaani Ubaguzi wa Rangi Dhidi ya Waafrika


Wizara ya Mambo ya Nje ya China imekemea vitendo vya unyanyasi na ubaguzi dhidi ya waafrika wanaoishi kusini mwa China katika jimbo la Guangdong, na imesema kwamba serikali ya China itaendelea kuhakikisha raia wote wa kigeni wanapatiwa haki sawa nchini humo.

China imesema haya baada ya video na picha kuzagaa kwenye mitandao ya jamii ikiwaonyesha waafrika wengi wakiwa wamezagaa mitaani katika maeneo mbalimbali nchini China wakiwa na mabegi ya nguo wakidai wamefukuzwa kwenye nyumba zao na mahotelini.

Taarifa zaidi zimedai kwamba vitendo hivyo vya kinyume na haki za binadamu vimekuwa vikifanywa na mamlaka za serikali ya China ambazo zinawashutumu raia wa kigeni hususani waafrika kwamba wanasambaza ugonjwa wa corona nchini humo.

“Tunapitia changamoto nyingi kwani tumejifungia ndani kwa takribani miezi mitatu. Changamoto kubwa ni ubaguzi wa rangi kwani imefikia wakati sasa haturuhusiwi kupata huduma za afya katika mahospitali..” alisema mmoja wa waafrika ambaye kwa sasa anaishi nchini China wakati wa mahojiano kupitia televisheni ya nchini Uganda.

Taarifa zaidi zinaeleza kwamba, waafrika wanaoshi nchini China hawaruhusiwi kununua bidhaa kama chakula katika masoko makubwa na pia wanazuiliwa kula katika migahawa nchini humo.

Akijibu tuhuma hizo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje nchini China, Zhao Lijian, alisema “Tangu mlipuko wa corona, China na nchi za Afrika zimekuwa zikishirikiana kupigana na ugonjwa huu. Hivyo hatuwezi kusahau msaada uliotolewa na nchi za Afrika wakati ambapo tulikuwa tumeathirika zaidi na ugonjwa huu,” alisema msemaji huyo kwenye barua ambayo ilitolewa kwa gazeti la Mwananchi na Ubalozi wa China nchini Tanzania.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad