Serikali yatangaza bei ya sukari, yatoa onyo kali kwa wafanyabiashara




SERIKALI imetangaza bei kikomo ya sukari nchini ambapo bei ya rejareja haitazidi Sh 2600 kwa mikoa ya karibu kama Dar es Salaam na Sh 3200 kwa mikoa ya mbali kama Katavi.

Akitangaza bei hizo leo jijini Dodoma, Waziri wa Kilimo, Joseph Hasunga amesema bei hizo zimezingatia umbali wa kila eneo katika mikoa yote nchini.

Hasunga amesema serikali imefikia hatua hiyo baada ya kubaini kuwa wafanyabiashara wa sukari wamepandisha bei kiholela kinyume na utaratibu huku akitoa onyo kali kwa ambaye atakaidi bei iliyotolewa.

" Tunawatangazia wafanyabiashara wote wenye tabia ya kupandisha bei kiholela kuacha mara moja kwani serikali haipo tayari kuona wananchi wake wanaumia kwa manufaa ya watu wachache.

Tutachukua hatua kali kwa mfanyabiashara ambaye atabainika kujinufaisha kwa kuuza sukari bei ya juu kuliko ya kawaida ya soko," Amesema Hasunga.

Hasunga amesema mfanyabiashara atakaekiuka maagizo hayo atakua ametenda kosa na hivyo kufikishwa katika vyombo vya sheria ili apate adhabu ambayo itahusisha kumnyang'anya leseni ya biashara au kulipa faini au adhabu zote kwa pamoja.

Waziri Hasunga amesema wafanyabiashara hao walidhani kutokana na viwanda vingi kushindwa kuzalisha sukari ya kutosha na uwepo wa ugonjwa wa Corona sukari ya kuziba pengo haitopatikana kirahisi hivyo wakaanza kujinufaisha wao kwanza.

Kwa upande wake Waziri wa Biashara na Viwanda, Innocent Bashungwa ametoa onyo pia kwa wafanyabiashara ambao watapandisha bei ya sukari huku akiiagiza tume ya ushindani FCC kushirikiana na Bodi ya Sukari kupanga bei ya jumla ya sukari.

" Serikali haitomvumilia yoyote ambaye atakaidi agizo la bei ya maelekezo lililotolewa, kwa wafanyabiashara wote wanapaswa kuteleleza agizo hili kwani limezingatia vigezo na gharama zote ambazo wanazitumia," Amesema Bashungwa.

Bei za sukari ni kama ifuatavyo, Iringa (2900), Mbeya (3,000), Rukwa, Katavi, Ruvuma (3,200), Njombe (2,900), Lindi, Mtwara (2,800), Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga (2,700), Dar (2,600), Pwani, Morogoro (2,700), Kagera, Mwanza, Shinyanga,Simiyu, Geita (2,900), Mara (3,000), Kigoma (3,200), Singida, Tabora, Dodoma (2,900), Songwe (3,000).
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Asante Waziri.

    wasituumize katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

    sukari ni Muhimu katika Futari zetu.

    Mungu akubarikini Sana. ktk uongozi wa hii awamu isiyo ya mchezo mchezo.

    Mungu akulinde JPJM. amin.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad