TMA imetoa Ufafanuzi Kuhusu Anga Kuonekana na Rangi Nyekundu au Chungwa Nchini



Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) imetoa ufafanuzi kuhusu anga kuonekana kuwa na rangi juzi huku wakieleza kuwa jambo hilo ni la kawaida hutokea wakati jua linapozama au kuchomoza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Aprili 17, 2020 imeeleza kumekuwa na hali ya taharuki na maswali kutoka kwa umma kuwa Aprili 16, 2020 majira ya jioni kuhusu mwonekano wa anga kuwa na rangi nyekundu au chungwa katika baadhi ya maeneo nchini.

“Mwonekano huo wa rangi la anga ni hali ya kawaida ambayo hutokea wakati jua linapozama au kuchomoza katika mazingira yenye kuwa na hali ya hewa kama vile mawingu, matone madogo madogo ya maji na barafu katika anga mara mvua inapokatika na jua linapokuwa katika upande tofauti na eneo mvua inaponyesha,”

“Hali ambayo husababisha kutawanywa kwa miale ya mwanga wa jua. Hivyo kutokana na ukubwa wa matone ya maji katika wingu na chembechembe za vumbi katika anga, sehemu ya miale ya jua inayotawanywa zaidi katika mazingira hayo ni mawimbi ya miale ya jua inayohusiana na rangi nyekundu au chungwa hivyo kufanya anga kuonekana katika rangi hizo (Mawimbi madogo sana huwakilisha rangi ya blue na makubwa rangi nyekundu au rangi ya chungwa).

Taarifa hiyo imeeleza kuwa hali hiyo haina tofauti sana na namna Upinde mvua unavyojitokeza angani, isipokuwa upinde mvua unakuwa na rangi zote saba za spectrum ya mwanga.

TMA imeeleza mabadiliko hayo ya hali ya anga hayana madhara yeyote.

Katika hali iliyozoeleka mara nyingi, anga huonekana kuwa rangi ya bluu kutokana na kutawanywa kwa mawimbi ya miale ya jua kunakofanywa na gesi ya Nitrojeni na Oksijeni ambazo ndizo hufanya sehemu kubwa ya gesi katika hewa.

Hali hiyo inatokana na molekuli za gesi hizo kuwa ni ndogo sana hivyo hutawanya sehemu ya mawimbi madogo zaidi ya miale ya jua iliyo katika rangi ya blue katika spectrum ya mwanga. Rangi hiyo huonekana katika macho ya binadamu kwa kipindi hicho

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad