Tundu Lissu Amshangaa Spika Kuhusu Madai yake
0
April 08, 2020
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amedai kuwa bado hajalipwa ‘gratuity’ (bahkshishi) yake ambayo ni asilimia 40 ya mshahara wake, tofauti na kile kinachoelezwa bungeni.
Lissu amesema hayo ikiwa ni siku chache baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai, kulieleza kuwa Lissu ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, hadai chochote na kwamba ameshalipwa madai yake yote.
Vile vile, alidokeza kuwa mwanasiasa huyo anadaiwa Sh. milioni 70 ya mikopo aliyokopa benki. Akizungumza na Nipashe akiwa nchini Ubeligiji, alihoji: “Niliuliza swali dogo tu, je, nimelipwa kiinua mgongo changu ambacho ni sawa na asilimia 40 ya mishahara yangu?”
“Hayo ya mikopo yangu ya benki yana uhusiano gani na madai yangu ya ‘gratuity’, hakuna uhusiano hapo,” alisema.
Juzi Spika wa bunge, Ndugai, alieleza kuhusu fedha ambazo Bunge limemlipa Lissu ikiwamo posho mbalimbali na mishahara zaidi ya Sh. milioni 500 na kusema kuwa kwa sasa hana madai yoyote anayodai Bunge isipokuwa yeye (Lissu) ndiye anayedaiwa mikopo aliyodai kupitia bunge hilo inayofikia Sh. milioni 70 ambayo bado hajalipa.
“Lissu anapenda sana kuzungumza mambo yake mbele ya jamii, mimi nadhani si busara tena anachokizungumza hakina ukweli ni vyema angepiga hesabu vizuri,“ alisema Spika Ndugai.
Tangu kuvuliwa ubunge kwa kiongozi huyo wa Chadema, pamekuwa na mvutano kati yake na Bunge kuhusiana na madai mbalimbali ambayo aliyaibua Lissu ikiwamo mishahara, posho na fedha za matibabu wakati mwanasiasa huyo akidai kuwa ni haki yake kulipwa madai hayo Spika wa Bunge, amekuwa akisisitiza kuwa hakuna anachokidai katika bunge hilo.
Lissu alipigwa risasi 32 kati yake tano zilimpata mwilini Septemba 7, 2017, alipelekwa jijini Nairobi kwa ajili ya matibabu na baadaye nchini Ubeligiji ambako amekuwapo hadi sasa.
Tags