Utajiri wa Mama Rwakatare Ngoma Nzito!


KIFO cha ghafla cha Mchungaji Kiongozi, Askofu Dk Getrude Rwakatare ‘Mama Rwakatare’ wa Makanisa ya Mlima wa Moto (Assemblies of God) yenye makao yake makuu Mikocheni B jijini Dar, kimeshtua wengi, lakini kubwa ni juu ya utajiri mkubwa aliouacha.

Imeelezwa kuwa, utamaduni wa kuandika wosia kwa Watanzania bado haujawaingia akilini watu wengi hivyo jambo hilo linafikirisha pia juu ya utajiri mkubwa aliouacha Mama Rwakatare.

Mama Rwakatare alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi Jumatatu katika Hospitali ya Rabininsia iliyopo Tegeta jijini Dar kutokana na matatizo ya ghafla ya presha na moyo.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa gazeti ndugu la hili, Uwazi, hivi karibuni lilichapisha ripoti ya wachungaji matajiri Bongo na kuanika utajiri mkubwa alionao Mama Rwakatare.

Kwa mujibu wa Uwazi, Mama Rwakatare ni miongoni mwa watumishi wa Mungu waliofanikiwa kujenga majumba ya kifahari na kisasa jijini Dar.

Mahekalu hayo ya Mama Rwakatare yalitajwa kuwa, moja ipo Mikocheni B lilipo Kanisa la Mlima wa Moto likiwa na ghorofa moja na lingine kubwa la kifahari lipo ufukweni mwa Bahari ya Hindi huko Mbezi-Beach jijini Dar, likiwa na ghorofa moja.

Mama Rwakatare, mbali na kumiliki majumba hayo ya kifahari, pia anamiliki kituo cha Redio cha Praise Power na hivi karibuni alitarajia kuzindua kituo cha runinga kinachoitwa Ebenezer Televisheni.

Mbali na hivyo, pia anamiliki shule na vyuo vingi vya St Mary’s kwenye mikoa mbalimbali chini.

Mbali na hivyo, Mama Rwakatare anatajwa kumiliki mahoteli na biashara za vyakula na migodi ya madini.

Mbali na mabasi kibao yanayobeba waumini wake maelfu kuwapeleka kanisani na kuwarudisha majumbani, kwa mama Rwakatare ambaye alikuwa ni Mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya CCM lilikuwa ni jambo la kawaida sana kuendeshwa kwenye magari ya kifahari kama Toyota Land Cruiser V8 na mengine mengi.

KWA NINI NGOMA NZITO?

Kama Mama Rwakatare atakuwa hajaacha wosia au katika katiba haielezi vizuri umiliki wa Makanisa ya Mlima wa Moto na mali nyingi alizoacha na endapo busara ikashindwa kutumika, utajiri huo mkubwa aliokuwanao kiongozi huyo mkubwa wa dini, unaweza kuwa kaa la moto kwa wanaye wanne na wabia wake kwenye umiliki wa makanisa hayo.

TUWASIKILIZE WAOMBOLEZAJI

RISASI MCHANGANYIKO, juzi na jana lilifika nyumbani kwa Mama Rwakatare, Mbezi-Beach na kanisani kwake (Mikocheni B) kisha kuzungumza na baadhi ya waombolezaji ambao waliuelezea utajiri wa mama huyo.

“Kama hajaacha wosia hapa kazi ipo, angalia majumba aliyoacha, angalia magari ya kifahari, angalia makanisa yalivyotapakaa nchi nzima, angalia shule za St. Marry’s na vyuo vingi, angalia mashamba na makampuni ya mazao na hata madini, sasa hapa ngoma lazima iwe nzito kama hakuweka mambo sawa,” alisema mmoja wa waombolezaji katika mazungumzo na mwandishi wetu kanisani hapo Mikocheni B.

“Suala la msingi ambalo linaweza kunusuru kusitokee matatizo yoyote katika hili, basi ni iwe mama ameandika wosia kabla hajafariki dunia.

“Ninavyomjua Mama Rwakatare kutokana na kuwa alikuwa na jopo la wanasheria, kwa vyovyote vile haiwezekani akawa amefariki dunia bila kuandika wosia,” alisema mwombolezaji mwingine.

WACHUNGAJI 12

Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kwamba, Kanisa la Mlima wa Moto lilikuwa likiongozwa na Mama Rwakatare, lakini nyuma yake kukiwa na wachungaji 12 (thenashara) ambao haifahamiki kama ni sehemu ya wabia wa umiliki wa makanisa hayo.

WATOTO WA MAMA RWAKATARE

Hadi umauti unamkuta, Mama Rwakatare ameacha watoto wanne; Rose Rwakatare, Tibe Rwakatare, Mutta Rwakatare na Humphrey Rwakatare ambao kama wosia hautakuwa umeweka mambo sawa, basi moto utawaka.

KUHUSU MAKANISA YA MLIMA WA MOTO

Baadhi ya wachungaji waliozungumza na gazeti hili kwa ombi la kutotajwa majina, walitahadharisha kwenye makanisa ya Mlima wa Moto kusije kukatokea kile kilichotokea kwenye Makanisa ya Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), mara tu baada ya kifo cha Askofu Mkuu, Dk Moses Kulola kilichotokea Agosti 29, 2013 ambapo wachungaji walifikia hatua ya kufikishana mahakamani.

HISTORIA YA MAMA RWAKATARE

Historia ya marehemu Dk. Rwakatare inasisimua sana! Kwa kipindi kirefu amekuwa kielelezo cha mwanamke jasiri, aliyepambana kutoka kwenye sifuri, hadi kufikia kuwa na ukwasi mkubwa, akiwa ni kiongozi mkubwa wa dini, mbunge, mjasiriamali na mhamasishaji mkubwa katika jamii.

“Leo ninayo furaha ya kipekee kwa kutunukiwa tuzo ya heshima kwa ajili ya utumishi bora wa kiroho na hata kwa jamii! Tuzo hii imetokana na watu hao kunifuatilia kwa kipindi chote cha tangu nasoma Marekani nasomea uchungaji, nilivyorudi na kufanya kazi mbalimbali, shule nilizoanzisha, nilivyowasaidia akina mama na jinsi nilivyoweza kuanzisha kanisa, nilianza mwenyewe kwa moyo wa kupenda na mpaka makanisa yakapendeza na kuenea nchi nzima.

“Kwa Afrika Mashariki, ninayo furaja kusema kwamba mimi ndiye wa kwanza kupewa tuzo hii, hajawahi kupewa mtu mwingine yeyote, mimi ndiye wa kwanza, kwa hiyo nashukuru sana!”

Hayo ni maneno ya Mchungaji, Dk Getrude Rwakatare aliyoyatoa wakati akipokea tuzo maalum, aliyotunukiwa na Umoja wa Wachungaji na Maaskofu Duniani (International Communion of Charismatic and Evangelical Bishop Inc) wenye makao makuu yake Washington DC nchini Marekani.

Kama alivyosema mwenyewe, kwa Afrika Mashariki, Mama Rwakatare ndiye wa kwanza kupewa tuzo hiyo ya heshima ambayo hujulikana kama Certificate Of Meritorious Service Award.

Pengine unaweza kujiuliza, mama Rwakatare ni nani hasa mpaka kustahili tuzo hii? Amefanya nini katika utumishi wake wa kiroho na kijamii mpaka sifa zake zikaenea dunia nzima na kusababisha apate tuzo? Majibu yote utayapata hapa.

MAMA RWAKATARE NI NANI?

Mama Rwakatare alizaliwa Desemba 31, 1950 yapata miaka 70 iliyopita huko Ifakara mkoani Morogoro.

Alisoma Shule ya Msingi Ifakara, akajiunga na Sekondari ya Korogwe hadi kidato sita.

Baadaye alijiunga na Chuo cha North London Polytechnic nchini Uingereza. Baadaye alijiunga tena na Chuo cha Eastern and Southern Africa Management Institute alikopata shahada ya kwanza ya mawasiliano ya umma (Bachelor Degree in Mass Communication).

Safari yake ya kitaaluma haikuishia hapo kwani alikwenda Chicago, Illinois nchini Marekani alikojiunga na Chuo Kikuu cha Kikristo cha Moody ambako huko ndiko msingi wake wa mambo ya kichungaji ulipojengeka na kumfanya kuwa Mama Rwakatare.

Safari ya kielimu, iliendelea na kumfanya kuzidi kupanda ngazi moja ya kitaaluma hadi nyingine, hadi kufikia hatua ya udaktari wa falsafa (Philosophy Doctorate- PhD) na kulifanya jina lake sasa libadilike na kuwa Dokta Getrude Pangalile.

Pengine utajiuliza jina la Rwakatare limetoka wapi wakati alizaliwa akiwa anaitwa Getrude Pangalile? Jina hilo lilitoka kwa mumewe, Kennedy Rwakatare. Walipooana, ndipo jina lake likabadilika na kuwa Getrude Pangalile Rwakatare. Kwa bahati mbaya, mumewe huyo alifariki dunia mwishoni mwa mwezi Machi, 2013 Bukoba mkoani Kagera.

AJIRA

Ajira ya kwanza ya Mama Rwakatare aliporejea nchini, ilikuwa ni katika Mamlaka ya Bandari ya Afrika Mashariki (East Africa Harbours Authority) ambako aliajiriwa kuanzia mwaka 1984 na kuendelea na kazi hiyo hadi alipoamua kujiajiri mwenyewe kwenye ajira binafsi.

Ni hapo ndipo alipoanzisha shule ya kwanza ya St Mary’s, miongoni mwa shule za mwanzo kabisa nchini kufundisha kwa kutumia mtaala wa Kingereza (English Medium), akiwa ndiyo mkurugenzi wake.

Katika kipindi chote hiki cha ajira yake, mama Rwakatare alikuwa akiendelea na harakati za kidini, akiwa anahubiri neno la Mungu.

Mbali na maombezi na huduma nyingine za Neno la Mungu, Mama Rwakatare amekuwa mwalimu mzuri wa masomo ya ndoa, ujasiriamali na changamoto mbalimbali za kimaisha na amefikia hatua ya kuwa anatoa hadi mikopo kwa wanawake waumini kanisani kwake na wasio waumini, kwa ajili ya kuanzisha miradi mbalimbali ya kuwakwamua kimaisha.

WAKATI huohuo, juzi Askofu Datsan Maboya ambaye ni Kiongozi Mkuu wa Maaskofu wa Makanisa ya Kipentekoste nchini aliliambia Risasi Mchangayiko kwa niaba ya kanisa kuwa mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa leo.

“Chukua hili kama dokezo kuu kwamba ikiwezekana mama atazikwa Alhamisi baada ya makubaliano ya pande tatu.

“Unajua mama alikuwa mtumishi wa serikali kwa maana ya ubunge, kiongozi wa kiroho lakini pia ni mama wa familia,” alisema Askofu Maboya.


“Kikao chetu kimemalizika, tunampelekea taarifa spika (Job Ndugai) ili aone namna ya kupanga ratiba za mazishi lakini kama itampendeza Mungu mama atazikwa hapa Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa, habari zozote zinazoenezwa mitandaoni zinatakiwa kupuuzwa na kuwashauri watu kuacha kuzua taharuki katika kipindi hiki cha janga la Corona.

STORI | Richard Bukos, Risasi
GPL

Post a Comment

2 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad