Vyama vya Siasa Zanzibar Vyakerwa na Kauli ya Maalim SEIF na Kuiomba Ofisi ya Msajili Kumchukilia Hatua
0
April 04, 2020
Viongozi wa Vyama vya Siasa Nchini wamelaani kauli zilizotolewa na Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo,Maalim Seif Sharif Hamadi kwa kuishutumu Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Inashirikiana na Baraza la Wawakilishi kutaka kutunga sheria itakayo weka masharti kwa mgombea wa urais.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Chama cha Cha Demokrasia Makini Ameir Hassan Ameir kwa niaba ya viongozi wa Vyama vya Upinzani Nchini, Tamko hilo limetolewa katika ukumbi wa Sanaa, Raha leo Mjini Unguja.
TAMKO LA VIONGOZI WA VYAMA VYA SIASA ZANZIBAR KWA WANAHABARI KUHUSIANA NA MAMBO MBALIMBALI YANAYOENDELEA NCHINI, LEO TAREHE 4, APRILI, 2020
Ndugu wanahabari Asalaam Alaaikum,
Kwanza poleni sana na majukumu mazito yanayowakabili katika kuwahabarisha wananchi juu ya matukio mbalimbali yanayotokea nchini, lakini pia, tunawapongeza kwa kazi nzuri mnayoendelea kuifanya hususani katika kuwahabarisha wananchi mambo mbalimbali ya Maendeleo, kiuchumi na kijamii yanayofanywa na Serikali yetu ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Mheshimiwa Dk. Ali Mohamed Shein. Hongereni sana.
Ndugu Wanahabari,
Sisi viongozi wa vyama vya siasa tumejitokeza kwenu kuelezea kufurahishwa na hali ya amani na Utulivu iliyopo nchini ambayo inatoa nafasi kwa wananchi kufanya shughuli zao za kimaendeleo, kiuchumi na kijamii bila matatizo na kubughudhiwa.
Pia tunaipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya Dk. Ali Mohamed Shein kwa kutatua kero mbalimbali zinazojitokeza nchini kwa haraka na kwa maslahi ya wananchi wote ili nchi yetu iendelee kudumu kwenye amani, utulivu na kufikia maendeleo kwa kasi.
Sisi viongozi wa vyama vya siasa tunawapongeza wananchi kwa kutuunga mkono na kuwa bega kwa bega katika kipindi chote na huu ni uthibitisho kwamba wananchi wanaondokana na siasa za chuki na uhasama na kujikita zaidi katika siasa za kuleta maendeleo ya nchi yetu.
Ndugu Wanahabari,
Kama mnavyofahamu, tunaelekea kwenye Uchaguzi Mkuu hapo Oktoba mwaka huu na hivi karibuni katika nchi yetu kulifanyika zoezi muhimu la utoaji vitambulisho vya Mzanzibari Mkaazi pamoja na uhakiki wa Wapiga kura katika Dafari la Kudumu la Wapiga Kura, lakini zoezi hilo liliingia dosari, za hapa na pale. Sisi viongozi wa vyama vya siasa tunalaani wale wote waliohusika na kitendo cha kutaka kuharibu kwa makusudi zoezi zima la uandikishaji la wapiga kura wapya na uhakiki wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Tunapongeza hatua zilizochukuliwa na Serikali anayoiongoza Dk. Ali Mohamed Shein kwa baadhi ya watendaji.
Ndugu wanahabari,
Pamoja na hatua zilizokwishachukuliwa na Serikali, katika kudhibiti dosari hiyo, Sisi viongozi wa vyama vya siasa tunawataka wale wote waliopewa jukumu la kusimamia utendaji wa zoezi hili kuhakikisha wanafanya kazi zao kwa weledi na uzalendo mkubwa ili kuiepusha nchi kuingia kwenye dhahma, kwani lolote litakalotokea wao ndio watawajibika.
Tunaviomba vyombo husika vya utafiti wa mwenendo wa kisiasa pamoja na vyombo vya kutekeleza sheria kuishauri Serikali mara moja inapotokea mambo yanayoleta viashiria vinavyotaka kuteteresha Umoja wa Wananchi, Maendeleo, Uchumi, Jamii, amani na utulivu wetu kwa jumla.
Hata hivyo, Sisi viongozi wa Vyama vya Siasa tunamshauri Msajili wa Vyama vya Siasa kufanya utafiti wa kina katika masuala yanayojiri Zanzibar, ikiwemo harakati za kisiasa na mwenendo wake, kwa sababu uchaguzi unaanza mapema sana kwa kutoa elimu, uandikishaji, kampeni upigaji kura pamoja na matokeo ya upigaji kura.
Haitokuwa na maana hata kidogo kusubiri matokeo ya uvunjifu wa sheria na amani kwa sababu kinga ni bora kuliko tiba.
Sisi tunaamini chama chenye mustakabali unaoendana na sheria za vyama vya siasa kinajidhihirisha matendo yake wakati wote na sio wakati wa matokeo ya kura pekee kwa kuweka rehani hisia za wananchi.
Kauli za uchochezi
Ndugu Wanahabari,
Sisi viongozi wa vyama vya siasa tunalaani kwa nguvu zote kauli zilizopata kutolewa na Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad kuishutumu Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kwamba inashirikiana na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kutaka kutunga sheria ambayo itaweka masharti anayetaka kugombea Urais wa Zanzibar, lazima awe mwanachama wa Chama Cha Siasa kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu na hivyo, kutaka kumzuia yeye asigombee katika Uchaguzi MKuu ujao wa mwaka huu.
Ameishutumu Tume ya Uchaguzi (ZEC) na CCM kuwa kinashirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuzuia uchaguzi Mkuu ujao wa 2020 usifanyike kwa amani na utulivu. Aidha ameitishia Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwamba wao sasa wako tayari kwa lolote litakalotokea.
Mwenyekiti huyo wa ACT- kwa nyakati tofauti amekishutumu Chama Cha Mapinduzi kwamba kimeandaa makundi kukihujumu chama chake. Makundi hayo aliyoyaita ya kihuni yametiliwa nguvu zaidi wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally aliyoifanya Mwezi Oktoba, 2019.
Aidha amemshutumu Dkt. Bashiru kwamba alikuja Zanzibar kuleta vurugu na chuki dhidi ya Wazanzibar.
Kibaya zaidi Mwanasiasa huyo amehamasisha wafuasi wake kwa kutoa kauli za uchochezi na kuwataka kujitayarisha kubeba silaha za kijadi ikiwamo mawe, mapanga na mikuki na kuwa tayari kujibu mapigo endapo watashambuliwa.
Ndugu wanahabari,
Kama hiyo haitoshi, amewashutumu viongozi wa juu wa kitaifa kuwa wanashirikiana na Profesa Ibrahim Lipumba wa Chama Cha Wananchi (CUF) katika masuala ya kuleta vurugu za kisiasa na eti Chama Cha Mapinduzi kinapanga njama za watu kuuwana katika kisiwa cha Pemba, aidha ameidhalilisha Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuiita Serikali haramu na kuhoji juu ya uhalalali wake na kusisitiza kutoitambua.
Kiongozi huyo aliendelea kutoa kauli za vitisho zinazoashiria Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020 kuwa hautofanyika mpaka yeye ahalalishwe. Kauli hizo zinazo tafsiri moja na swali moja kwamba kiongozi huyu anayo siri ipi na mustakabali gani juu ya amani na demokrasia kwa wananchi wa Zanzibar?
Ndugu wanahabari,
Matukio hayo pamoja na kauli za uchochezi zinazotamkwa na kiongozi huyo zinaashiria uvunjifu wa amani, kujenga chuki, uhasama na kuleta vurugu miongoni mwa Wazanzibar.
Sisi viongozi wa vyama vya siasa tunaamini shutuma za kiongozi huyo hazina ushahidi wowote bali imekuwa ni tabia yake ambayo Wazanzibar wote wameshamgundua kwamba lengo lake ni kuona nchi yetu inaingia katika machafuko, vitisho, suala ambalo Wazanzibar hawaliungi mkono.
Ndugu wanahabari,
Sisi viongozi wa vyama vya siasa tunamuomba Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, kuzitathmini kauli hizo, athari na nia yake kwa Serikali na jamii kwa jumla. Na kwamba tunaomba Msajili kufanya utafiti wa kina na kuangalia uhalali wa chama hicho na kiongozi huyo kama bado hakijapoteza sifa za kuwa chama cha siasa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa nambari 5 ya mwaka 1992.
Ndugu Msajili wa Vyama vya Siasa kwanini sisi vyama vingine hatuoni hayo anayotamka Mwenyekiti wa Chama Cha ACT- Wazalendo? Bali tunaona mwenendo mzuri wa Serikali kwa kuwatakia wananchi wake maendeleo, huku ikinawirisha uwepo wa amani, mshikamano na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Tume Huru ya Uchaguzi:
Tunapenda kufafanua wazi na kuufahamisha umma kuwa, kabla ya kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi, Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein alituita sisi viongozi wa vyama vya siasa wa kitaifa, katika kikao cha pamoja Ikulu Zanzibar tulitoa maoni na mapendekezo yetu na kufikia maridhiano ya pamoja yenye muafaka kabla ya kutangazwa wajumbe wa Tume Huru ya Uchaguzi.
Tunalaani kauli za kiongozi huyo kwa kuupotosha umma kwa kutoa kauli ambayo ilifanyika katika kikao halali cha Kitaifa huku ikiwa mwenyewe hajahudhuria.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa:
Sisi viongozi wa vyama vya siasa kwa upande wa Zanzibar bado hatujaridhishwa kwa kiasi kikubwa katika ushirikishwaji mpana wa pamoja kwa vyama vyote vya siasa katika ujenzi wa taifa letu pamoja na serikali kwa ujumla.
Kwa maana hiyo tunaomba Serikali kuitisha tena kwa kura ya maoni (Referendum) kuhusu hatma ya mustakabali wa muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo tunataka itoe nafasi kwa kuvishirikisha vyama vyote vya siasa katika kuunda Serikali.
Tumeshuhudia kuwa kura ya maoni iliyopigwa mwaka 2000 na kutoa nafasi kwa vyama vya siasa vya CCM na CUF pekee havikuwa na ushiriki wa kitaifa na kwa maana hiyo tumeshuhudia wenzetu wakisusia baadhi ya harakati za Serikali, mipango ya maendeleo na hata uchaguzi wa marudio uliofanyika mwaka 2016.
Pia, yote haya yaliendelezwa kwa Chama cha CUF kususia Serikali na bajeti yake na kutoa matamko ya uhasama na kutotambua Serikali waliyoiunda wao wenyewe. Hivyo basi, tunaiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufanya utafiti suala hili kwa maslahi mapana ya Taifa letu.
Ilani ya uchaguzi CCM
Sisi viongozi wa vyama vya siasa tumefurahishwa na kuridhishwa na mwenendo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 inayosimamiwa na Rais wa Zanzibar na Makamo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.
Hata hivyo, tunawaomba watendaji wanaosimamia maeneo yote ambayo Ilani hiyo inatekelezwa kuhakikisha hawamuangushi Rais ambaye amekuwa mstari wa mbele kuboresha sekta ya Afya, Elimu, Ustawi wa jamii, Miundombinu ya barabara na miundombinu mingine mijini na vijijini. Kuhakikisha wanamaliza viporo kwa haraka ili kuendana na kasi ya Raisi.
Hongera sana Dk. Shein
Ugonjwa wa Corona
Ndugu wanahabari,
Kama tunavyofahamu ugonjwa wa corana umeenea duniani kote, kwa kauli moja tunapongeza juhudi zilizochukuliwa na zinazoendelea kuchukuliwa na viongozi wetu wakuu katika kupambana na ugonjwa huu wa homa ya mapafu corona (COVID 19) ambao ni janga la kimataifa.
Tunawaomba wananchi wawe watulivu huku wakifuata maelekezo yote yanayotolewa na viongozi wetu wakuu, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk.John Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein pamoja na wataalamu wa afya katika kujikinga na janga la corona kwani hadi sasa hakuna chanjo ya ugonjwa huo.
Pia tunaomba wananchi wote kujiepusha na vikundi visivyo vya lazima, kupeana mikono, kufanya safari zisizo za lazima sambamba na kunawa mikono kila baada ya nusu saa ili kuepusha maambukizo.
Ndugu wanahabari
Pamoja na maelekezo mbalimbali yanayotolewa na wataalamu juu ya kujikinga na ugonjwa huu, tunawataka viongozi waandamizi hususani wa kitaifa nao kuchukua tahadhari pale wanapotoka katika safari za kikazi nje ya nchi kuhakikisha wanafuata maelekezo ya wataalamu yanayowataka kufuata taratibu zote za kujikinga na ugonjwa ili usisambae ndani ya nchi.
Ndugu Wanahabari
Sisi viongozi wa vyama vya siasa tunachukua fursa hii kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi, kwa kutii amri ya wataalamu baada ya kurudi safari ya nje ya nchi alifuata taratibu za kitaalamu kwa kukaa siku 14 bila kukutana na mtu yeyote kwa lengo la kuchukua tahadhari kwa familia yake na wananchi kwa jumla ili kuepuka athari ambazo zingeweza kuepukika.
Ndugu wanahabari,
Sisi viongozi wa vyama vya Siasa Hata hivyo, tunaishauri Serikali kuchukua hatua ya kuweka karantini ya siku 21 hapa Zanzibar kwa nia njema ya kuhakikisha ugonjwa huu hauendelei kusambaa kwa wananchi. Sambamba katika kipindi hicho Wizara ya Afya ichukue hatua ya kupuliza dawa sehemu mbalimbali zilizo na mikusanyiko ya watu na kwenye maofisi mbalimbali
Ahsanteni sana kwa kutusikiliza
Tamko hili limetolewa na sisi viongozi wa vyama vya siasa vya
Demokrasia Makini
SAU
UPDP
NLD
DP
TLP
CCK
CCM
TADEA
AFP
NCCR- Mageuzi
ADC
Limesomwa kwenu na mimi Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia Makini Ameir Hassan Ameir kwa niaba ya viongozi wenzangu wa vyama vya Siasa nchini.
Tags