Makumi ya watu waliokuwa katika karantini ya lazima nchini Kenya wamefanya mgomo na kutishia kutoroka katika kituo hicho katika mji mkuu wa Nairobi.
Wanadai kwamba kusalia kwao katika vituo hivyo sio haki kwa kuwa wamepimwa mara mbili na kukosekana kuwa na virusi hivyo.
Wiki iliopita , serikali ilitangaza kwamba muda wao wa kusalia karantini utaongezwa kutoka wiki mbili hadi mwezi mmoja baada ya kupatikana wakikaidi baadhi ya maagizo ya serikali kukabiliana na virusi vya corona.
Lakini kati ya wale walio katika karantini wanasema kwamba wanaugua shinikizo la kiakili.
Kundi hilo la watu 21 ambalo limekuwa likiishi katika chuo kikuu cha KU liliagizwa kusalia baada ya vipimo vya hivi karibuni kuwapata wawili wao na virusi ..
Hatua hiyo inajiri huku Kenya ikiripoti wagonjwa wengine tisa wa virusi vya corona , na kufanya idadi ya wagonjwa waliopatikana na ugonjwa huo kufikia 225.
Kulingana na waziri wa Afya Mutahi Kagwe maambukizi hayo mapya yaliripotiwa baada ya sampuli 803 kufanyiwa vipimo katika kipindi cha saa 24 zilizopita.
Wagonjwa wote ni Wakenya . Hakuna aliye na historia ya kusafiri wala aliyetoka katika kituo cha karantini.
Wagonjwa watano wanatoka Nairobi huku wanne wakitoka Mombasa.
Wana kati ya umri wa miaka tisa na 69. Hatahivyo waziri Kagwe amesema kwamba kuna habari njema baada ya wagonjwa 12 kupona na kuachiliwa kurudi nyumbani hatua inayofanya idadi ya walipona kwa jumla kufikia watu 53.
Hatahivyo mgonjwa mmoja ameripotiwa kufariki na kuongeza idadi ya waliofariki kutokana na virusi hivyo kufikia watu 10.
Waziri huyo amesema kwamba takriban watu 2336 waliokaribiana na wagonjwa hao wanachunguzwa huku 455 kati yao wakifuatiliwa.
Kagwe siku ya Jumatano alisema kwamba kaunti zimewekwa katika hali ya tahadhari na kwamba maafisa wamepelekwa Siaya wakiongozwa na mkurugenzi mkuu wa wa Afya Dr Patrick Amoth.
Kundi hilo lilikaguwa vituo vya kujitenga vilivyowekwa.
Pia serikali ilipeleka vifaa vya wafanyikazi wa Afya.
''Vita hivi vitashindwa na Wakenya watakaofanya kazi pamoja… sio jukumu la serikali'', Kagwe alisema.
Serikali pia ilisema kwamba imepokea vifaa vya kukabiliana na virusi hivyo kutoka kwa wakfu wa Jack Ma na shirika la afya Duniani WHO.
''Bado hatujajiondoa katika hatari'', alisema Kagwe.
Waziri huyo pia aliwashutumu Wakenya wasioshirikiana na maafisa wa polisi kuzuia maambukizi.
Waziri huyo aliwataka wanaharakati wa haki za kibinadamu kutowatetea raia bali pia maafisa wa polisi.
Aliwapongeza polisi kwa kuhakikisha kuwa amri ya kutotoka nje usiku inafuatwa.