Raia weusi wa mji wa Chicago ni nusu ya visa vyote vya ugonjwa wa virusi vya corona katika mji huo
Takwimu kutoka maafisa wa afya mjini Chicago zimeonesha athari kubwa ya virusi vya corona katika Wamarekani weusi.
Raia weusi wa mji wa Chicago ni nusu ya visa vyote vya ugonjwa wa virusi vya corona katika mji huo na zaidi ya asilimia 70 ya vifo vyote , licha ya kwamba idadi yao ni asilimia 30 ya watu wote katika mji huo.
Miji mingine yenye idadi kubwa ya watu weusi ikiwemo Dteroit, Milwaukee , New Orleans na New York pia imetajwa kuwa maeneo yalio hatari.
Marekani imerekodi wagonjwa 370,000 wa virusi hivyo na takriban vifo 11,000. Kote duniani kumekuwa na vifo 75,000 na visa milioni 1.3 kwa jumla.
Je takwimu hizo za Chicago zinaonesha nini?
Kufikia tarehe 5 mwezi Aprili , visa 1,824 vya ugonjwa wa corona kati ya 4,680 vilivyothibitishwa vilihusisha wakaazi weusi, walisema maafisa wa mji huo siku ya Jumatatu.
Hiyo ni tofauti na visa 847 vya weupe, 478 vya Hispanic na 126 vya Wa - Asia wa Chicago. Chicago iliripoti vifo 78 siku ya Jumapili huku asilimia 72 ya vifo hivyo vikihusisha watu weusi.
Utofauti huo unaonekana katika jimbo zima, ambapo watu weusi ni asilimia 41 ya vifo vilivyotokana na Covid-19, licha ya kuwa ni asilimia 14 ya watu wote wa jimbo la Illinois.
Kamishna wa Afya ya Umma wa jiji la Chicago Dkt Allison Arwady amewaambia wanahabari kuwa wakaazi weusi wa jiji hilo tayari wana wastani wa maisha mafupi kwa miaka 8.8 kulinganisha na wazungu.
Meya Lori Lightfoot amesaema kuwa virusi vya corona "vitateketeza Chicago ya watu weusi".
Amesema kuwa wakaguzi wa jiji hilo watatumwa madukani kuhakikisha kila mtu anatekeleza maelekezo ya kujitenga kwa umbali na wengine.
Meya Lightfoot pia ameelezea juu ya uwezekano wa kuwekwa marufuku ya kutoka nje kwa baadhi ya saa katika maeneo ambayo watu hukusanyika kwenye maduka ya pombe, linaripoti gazeti la Chicago Sun-Times.
Taswira ipoje nchi nzima?Japo virusi vya corona vimepewa jina la "msawazo mkuu ", takwimu zinaonesha kuwa madhara ya maambukizi yanaweza kutofautiana kwa sehemu.
Katika jimbo la Michigan, Wamarekani Weusi ni asilimia 14 ya watu wote, lakini wao ni asilimia 33 ya wagonjwa wa corona na asilimia 41 ya vifo kutokana na ugonjwa huo, zinaonesha takwimu kutoka idara ya afya ya jimbo hilo kufikia jana Jumatatu.
Wazungu katika jimbo hilo ni asilimia 23 ya wagonjwa na vifo vyao ni asilimia 28, kwa mujibu wa takwimu hizo.
Jiji la Detroit
katika jimbo la Michigan, lina wakazi weusi takribani asilimia 80, na jiji hilo pekee pamoja na viunga vya karibu yake vina asilimia 80 ya wagonjwa wote wa corona katika jimbo hilo.
Utofauti kama huo pia unaonekana jiji la Milwaukee, jimboni Wisconsin, moja ya maeneo yaliyoathirika zaidi na ubaguzi wa rangi nchini Marekani.
Watu weusi kufikia Ijumaa ya wiki iliyopita wanafikia nusu ya wagonjwa 1,000 na asilimia 81 ya vifo, japo watu weusi ni asilimia 26 tu ya wakaazi wa jiji hilo.
Takribani asilimia 40 ya vifo vitokanavyo na virusi vya corona katika jimbo la Louisiana katika jiji la New Orleans ambako watu weusi ni wengi zaidi.
Maafisa wa Afya hapo awali walieleza kuwa wakaazi wengi wa New Orleans wanakabiliwa na matatizo ya unene wa kupitiliza, kisukari na presha ya kupanda kwa kiwango cha juu zaidi nchini Marekani hali inayowafanya kuwa rahisi kudhurika zaidi na Covid-19.
Utofauti wa Chicago unachochewa na nini?Meya Lightfoot anasema kisukari, magonjwa ya moyo na magonjwa ya mfumo wa hewa yapo "kwa kiwango kikubwa" kwenye jamii za weusi.
Dkt Arwady amewaambia waandishi kuwa hata kama kila mtu katika jiji hilo angekuwa na uwezekano wa kumuona daktari, "bado tungeendelea kuona utofauti mkubwa kutokana na upatikanaji haba wa chakula bora na mitaa ya kutembea ".
Dkt Cameron Webb, ambaye ni tabibu mweusi anayewania ubunge katika jimbo la Virginia, ameiambia BBC kuwa tofauti za rangi na kiuchumi zinaoneshwa wazi na janga hili.
"(Janga la corona) linaonesha nyufa za jamii yetu," amesema.
Alderman Jason Ervin, ambaye ni mwenyekiti wa umoja wa wawakilishi weusi katika baraza la jiji la Chicago ameliambia gazeti la Chicago Tribune kuwa "wingi wa watu wasiofuata maagizo ya kujitenga nyumbani katika baadhi ya sehemu za jiji hilo" inawezekana pia ikawa inachangia takwimu hizo.