Wakati dunia ikiendelea kupambana na virusi vipya vya corona (covid-19), wataalam wameeleza kuwa itachukua muda mrefu kidogo hadi kufanikisha kupatikana kwa dawa ya virusi hivyo.
Machi 20, 2020, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilieleza kuwa kuna dawa takribani 44 zinazoendelea kutengenezwa zenye matarajio ya kutibu au kuwa kinga dhidi ya virusi hivyo, ambazo zitajaribiwa kutafuta idhini.
Makampuni 35 na taasisi za elimu ziko kwenye mchakato wa kutafuta dawa, na dawa nne zimeshafanyiwa majaribio kwenye wanyama. Dawa ya kwanza ilitengenezwa na Kampuni ya Moderna ya Boston, ambayo inatarajiwa kufanyiwa majaribio kwenye mwili wa binadamu hivi karibuni.
Kwa mujibu wa Aljazeera, wanasayansi wabobezi wameeleza kuwa itachukua kati ya miezi 12 hadi 18 kupata dawa ya virusi hiyo, kupitishwa na kuanza kutumika rasmi.
“Baadhi ya dawa huchukua hadi miaka kumi au zaidi hadi kupitishwa na kupewa leseni ya kutumika. Hivyo, hata kufanikisha kupata dawa ya covid-19 ndani ya miezi 18 itakuwa ni hatua kubwa sana,” imeeleza taarifa ya Aljazeera.
Aidha, wanasayansi hao wameeleza kuwa dawa hiyo inaweza kugundulika mapema kwa sababu covid-19 ni sehemu ya kundi la virusi vya corona ambavyo vilikuwa vimeshafanyiwa tafiti nyingi awali.
Imeelezwa kuwa baadhi ya dawa za virusi vya corona aina ya SARS na MERS zilikuwa katika hatua ya mwisho ya kuombewa kibali, lakini baada ya kuibuka covid-19 mchakato huo ulisitishwa na wanasayansi wakajikita kuanza kusaka dawa ya virusi hivyo vipya.
Pia, imeeleza kuwa ingawa kuna majaribio ya dawa moja yanayofanywa nchini Marekani, ambayo yameruka hatua ya kufanya majaribio kwenye mnyama na kufanyika moja kwa moja kwa binadamu, hatua ya majaribio ya binadamu pia yanapaswa kupitia hatua tatu muhimu ambazo zitachukua muda.