Ndoa inatajwa kuwa ni elimu pekee ambayo mtu anapata cheti kabla ya kuingia darasani.
Licha ya misukosuko mingi iliyomo ndani yake ndoa imeendelea kuwa tukio muhimu katika jamii zote duniani na kurithishwa kwa vizazi na vizazi.
Moja ya misukosuko ya ndoa ni uaminifu, ambao baadhi yao wametokea kuukosa na kusababisha nyingine kuyumba au kufa kabisa.
Wataalamu kutoka maeneo mbalimbali duniani walijadili suala hili la hilo na kuja na dalili tano za wanandoa wasio waaminifu.
Kuchukia majukumu ya msingi ya ndoa
Watalaamu wanaeleza kuwa dalili mojawapo ni mwanandoa kutopenda kufanya mambo na kazi za familia.
Mtaalamu wa masuala ya ndoa kutoka Marekani Jeannie Ingram anayefanya shughuli za kutoa ushauri wa kindoa eneo la Nashville, Tennessee anasema zipo sababu nyingi za mmoja wa wanadoa kutoka nje ya ndoa, ikiwamo kutoshirikiana kwenye masuala mengi yakiwamo ya kifamilia.
Anasema mara nyingi mwanandoa anayetoka nje ya ndoa hana muda wa kusikiliza familia ina tatizo au furaha gani. Anafafanua kuwa hiyo inatokana na muda wote kufikiria mambo ya familia nyingine hata kama ni ya mtu huko alikoanzisha uhusiano.
“Akiwa anatoka nje ya ndoa hana muda wa kupoteza kufikiri vitu vingine zaidi ya mambo yake na jinsi atakavyokutana na mtu au watu wake anaoshirikiana nao kwenye usaliti, ” anasema Ingram.
Kuchukia kushiriki tendo la ndoa
Anasema wengi wao hufanya mapenzi na wenza wao kwa kujilazimisha na wakati mwingine kulazimishwa kwa uwazi kabisa.
“Wakiwa siyo waaminifu , hawavunjia pia uhusiano na wenza wao, aliliambia Jarida la HuffPost, ukweli ni kwamba uhusiano wa kindoa unahitaji kuimarishwamara kwa mara.
“Kukutana kimwili ni mojawapo ya mambo yanayopandisha mapenzi na kuamsha hisia ya kila mmoja wao kutamani kushiriki tendo hilo, jambo ambalo huwafanya kuwa pamoja muda wote ”anasema Ingram.
Wanatumia muda mwingi pamoja, lakini kila mmoja anafanya lake
Mtaalamu wa saikolojia kutoka Marekani Jimbo la Cororado Aaron Anderson anaitaja sababu ya kwanza kuwa ni pamoja na kutumia muda mwingi wakiwa pamoja, lakini kila mmoja ana shughuli zake ikiwamo kuchezea simu, kufungua kompyuta mpakato na kufanya kazi.
“Kama wewe na mke wako mnatumia muda mwingi katika chumba kimoja lakini kila mmoja ana shughuli zake na hakuna jambo lolote mnalojadili kuhusu uhusiano wenu mmoja au wote wawili mnatoka nje ya ndoa,” anasema Anderson.
Anasema siyo jambo la kawaida kwa wanandoa wanaopendana kutumia saa mbili kila mmoja akiperuzi kwenye mitandao ya kijamii.
Anasema kwa kawaida wapendanao wanapokaa wawili kila mmoja huzima simu, kompyuta na kuzungumza na mwenzake kwa namna yoyote ile.
“Hili halihitaji darubini huja lenyewe bila kufahamu, kuna ambao wakiwaona wenza wao husahau kila kitu , ”anasema.
Hawashirikiani katika mipango ya “mitoko” ya mwisho wa juma
Licha ya kuishi nyumba moja lakini kila mmoja hupanga mipango yake ya namna atakavyomaliza mapumziko ya wiki.
Mmoja wa wanandoa Said Miraji anasema kuwa alipomuoa mkewe ilikuwa kawaida mkewe kumlazimisha amsindikize hadi anapokwenda kutengeneza nywele.
Anasema baada ya kupata mtoto mmoja mambo hayo yalipungua na hatimaye kwisha kabisa.
“Nilipochunguza baada ya mambo ya kutaka kujitenga kuzidi, nilichobaini sitaki kusema, ninachoweza kukuambia ni kuwa ameolewa na mwanamume mwingine na ana watoto wawili na mimi kaniachia wawili ”anasema Miraji.
Kauli ya Miraji inaungwa mkono na mwanandoa mwingine Kuruthumu Rajabu anayesema kuwa mabadiliko yakitokea ndani ya ndoa mwisho wake ni kuachana.
Anasema baada ya kukaa kwenye ndoa na mumewe kwa miaka minne mwenza wake huyo alianza tabia ya kuchelewa kurudi isivyo kawaida.
Anasema mbali ya hilo, pia alikuwa hali chakula cha nyumbani, hajulikani anapumzika lini, kwa sababu kila siku anakwenda kazini, kibaya zaidi alikuwa hataki hata kuongozana naye.
“Ilifikia mahali hata nikimsubiri hatuwezi kwenda kulala pamoja lazima atatafuta kisingizio abaki sebuleni na kuja kulala kwa muda wake”anasema Kuruthumu.
Anasema licha ya kuwa mama bora, mcha Mungu, anayejali familia ya pande zote na kujaribu kuvumilia mapungufu ya mumewe, “Tuliishia kuachana, haikuwa kazi rahisi kumbadili alichoka manung’uniko yangu akaniacha”.
Hawaulizani hali, safari zinaongezeka
Anderson katika andiko lake alilochapisha kwenye jarida la Le wedding magazine la Ufaransa anasema kuwa ni nadra kwa mwanandoa anayetoka nje ya ndoa kumuuliza mwenzake habari za atokako hata kama amesafiri mwezi mzima.
“Anaweza asiulize hali za watoto pia bila kujali ni mwanamume au mwanamke, kwa sababu anawaza vitu vingine na kuchukia kwa nini aliolewa, ” anasema.
Anasema mwenza anayetoka nje ya ndoa muda mwingi anakuwa mtu wa safari za ndani au za nje ya eneo analoishi.
Huwasimanga au kuwasema vibaya marafiki, ndugu wa mwenza wake.
Kungwi maarufu Chausiku Salumu Maele maarufu Bi Chau anasema kuwa mbali na mabadiliko ya aina zote, kikubwa mwanandoa anayetoka nje ya ndoa huwachukia marafiki na ndugu wa mwenza wake.
Anasema anaweza kuwasema vibaya wakiwepo au pembeni.
“Huona kama wanaingilia uhuru wake wa kumbeza mume au mke, hivyo huwachukia na hutamani wasiwepo maisha.
“Ikitokea kwa bahati mbaya akapishana maneno ya mmoja wa watu hao kamwe hatomsamehe na huliweka hilo kama kosa kubwa maishani, ”anasema Bi Chau.
Anasema kuwa mwanandoa asiyemwaminifu pia huwa mgumu kujadili migongano ya ndani ya ndoa na akiulizwa hujibu “Sina muda wa kujadili suala hilo”.
Anasema kumsoma mwenza wako na kutambua mabadiliko ya tabia yake ni jambo muhimu ili kukwepa kuvunjika kwa ndoa.
Anafafanua hajawahi mwanaume au mwanamke kutoka nje ya ndoa na mpenzi mmoja kwa miaka miwili mfululizo na ndoa yake ikawa salama.
“Njia pekee ya kunusuru ndoa ni wanandoa kujuana tabia, kujibizana maswali panapotokea sintofahamu. Kukaa kimya na kupuuzia hisia kumekuwa chanzo kikubwa cha kuvunjika kwa ndoa nyingi, ”anasema Bi Chau.
Anachosema Bi Chau kinashadidiwa na Anderson anayesema mwanandoa anayetoka nje ya ndoa pia hana mapenzi na familia ya mmoja wao. Pia ndoa iliyoingia usaliti wanandoa huwasema vibaya marafiki wa wenza wao, kuwakashifu na kuwadhihaki.
“Ujue hapo hakuna ukweli kuna usaliti unaendelea kuwa makini, ”anasema Whetstone.
Mtaalamu wa saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Lusajo Kayula anasema kila ndoa au uhusiano una tabia yake ambayo wahusika wameizoea.
Anasema kwa sababu hiyo mabadiliko ya mwanandoa asiye mwaminifu hutegemea na mazoea yao.
Anafafanua kuwa dalili, tabia za mmoja kati yao anayetoka nje ya ndoa hulingana na walivyozoea ndiyo maana siyo rahisi kufanana kutoka ndoa moja na nyingine.
“Zipo tabia tofauti ambazo zinatia shaka ikiwamo kuwa makini na simu zaidi ya kawaida, kutotaka ukaribu na mwenza wake na kupoteza hamu ya tendo la ndoa kwa mwanandoa mwenza, ”anasema Kayula.
Kayula anafafanua kuwa zipo dalili nyingine ambazo mwanandoa anaweza kuwa nazo na bado asiwe anatoka nje ya ndoa.
Anafafanua kuwa wengi wanaamini mwanandoa anayechelewa kurudi nyumbani anakuwa na uhusiano, “Wapo wanaorudi saa 11 jioni na bado wanatoka nje ya ndoa, hicho siyo kigezo.
Anaeleza hata kupoteza hamu ya tendo la ndoa siyo kigezo kwa sababu wapo wanaopoteza kwa sababu ya msongo wa mawazo.
“Ndiyo maana nilisema hapo mwanzo hutegemea wahusika walizoea nini, kimetokea nini kwenye maisha yao, ”anasema.
Baadhi ya sababu za kutoka nje ya ndoa
Bi Chau anazitaja baadhi ya sababu za kutoka nje ya ndoa kuwa ni pamoja na wanandoa hususani wanawake kuaminishwa kuwa moja ya jukumu lao ni kuficha siri za ndani ya ndoa.
Anasema iwapo watatoka na kutafuta tiba ya matatizo mbalimbali yanayowakuta ndani ya ndoa hali hii haitakuwepo, “Sitaki kukudanganya tatizo la kutokuwa na nguvu za kiume limekuwa kubwa.
“Wanawake hawawezi kulalama kuhusu hilo matokeo yake wanakuwa watumwa wa ngono, wanaume nao halikadhalika, kutokana na kutoka nje ya ndoa wanapunguza mapenzi kwa wake zao na hatimaye kutotamani kukutana nao na kuwa watumwa wa mapenzi wa nje ya ndoa, ”anasema.
Anafafanua kuwa hizo ni baadhi ya sababu, zipo nyingi na zinahitaji kutafutiwa majibu na wanandoa wote.
“Kiukweli hili ni jinamizi, hakuna ambaye yupo salama, wanandoa wengi wanatoka nje ya ndoa zao, ili usiwe mmoja wao kuwa makini.
“Dawa ni kusema, kujadili kukubaliana , kueleweshana kwa pamoja badala ya kila mmoja kumuona mwenzake mkosaji, ”anasema.