Watiwa Mbaroni Kwa Tuhuma Za Mauaji Ya Mwalimu
0
April 13, 2020
Jeshi La Polisi mkoani Dodoma, linawashikilia watu watano kwa tuhuma za mauaji ya Mwalimu Eradius Lucas Mgaya wa Kijiji cha Chilungulu, Tarafa ya Bahi .
Hayo yalisemwa jana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto wakati akiongea na waandishi wa habari.
Alisema tukio hilo lilitokea Aprili 7, mwaka huu ambapo inadaiwa kuwa watuhumiwa hao watano (hakiwataja majina)walimpiga mwalimu huyo na kitu chenye ncha kali na kumtupa kwenye shamba la shule baada ya kumvizia njiani wakati akirejea nyumbani kwake .
“Bado tunaendelea kufanya uchunguzi kuhusiana na tukio la kifo cha Mwalimu Godfrey na tunaendelea kuwashikilia watuhumiwa wa mauaji hadi hapo uchunguzi utakapo kamilika,” alisema Kamanda Muroto.
Wakati huo huo Kamanda huyo wa Mkoa wa Dodoma aliwataka wenye magari kuchukua tahadhari kuhifadhi magari yao katika mazingira salama ikiwa ni pamoja na kuepuka kuegesha magari katika mazingira yanayowavutia wahalifu kuiba.
Alisema uchunguzi wa Jeshi la Polisi mkoani hapa umebaini kuwa magari yanayowaniwa zaidi ni yale yanayotumia funguo za ‘Sensor’ ambazo hazihitaji kuchongwa .
“Tunawashauri kuchukua tahadhari zote ikibidi wafunge Car truck system kwenye magari au CCTV kamera kuongeza utambuzi wa wahalifu baada ya matukio,”alisisitiza.
Aliwataka wenye magari kuwa makini na waosha magari, mafundi wao, madereva wanaotumia kusafirisha au kusafiri nao safari za mbali .
Tags