Waziri Bashungwa Afafanua Kuhusu Kupanda Kwa Bei ya Sukari


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa amewatoa hofu Watanzania kutokana na kupanda kwa bei ya sukari na kusema nchi imeagiza tani zaidi ya elfu 20 kutoka nje kama tahadhari ya kuwa na akiba katika kipindi hiki cha ugonjwa wa COVID-19.

Akizungumza na wanahabari jijini Dodoma, Mhe. Bashungwa amesema serikali inafanya jitihada za kuongeza uzalishaji wa sukari huku ikiwa imeunda tume ya wataalamu ili wafanyabiashara watakaobainika kuficha sukari wachukuliwe hatua kali.

Waziri Bashungwa amesema kuwa tayari sukari iliyokwisha ingia bandarini kupitia kampuni ya Kagera Sugar ni Tani 9,990 na imeanza kutolea bandarini tangu jana jioni.

Kadhalika tarehe 24, 28 na 30 kampuni ya Mtibwa Sugar itaingiza jumla ya tani 10,000. Kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza jumla tani 1,624 hivi karibuni kutoka Malawi na Msumbiji huku tani 1,800 ikiagizwa kutoka Afrika Kusini.

Sambamba na hayo amesema kuwa wiki ya kwanza ya mwezi Mei  Kampuni ya Kilombero Sugar itaingiza Tani 7,276 huku tarehe 15 Mei kampuni ya TPC itaingiza Tani 5,000 na Tarehe 30 Mei Tani 4,500 zitaingia nchini.

Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amesema kuwa Wizara inatarajia kuomba nyongeza ya Tani 58,000 ili kukidhi mahitaji ya sukari kufikia Juni 2020

Nao baadhi ya wakazi wa jiji la Dodoma wameiomba serikali kuchukua hatua za haraka kuhakikisha inadhibiti mfumuko wa bei ya sukari huku baadhi ya wafanyabiashara ndogondogo wakisema biashara zao zimeathirika.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad