Waziri mkuu akoshwa na jitihada za Ummy Mwalimu "Watanzania wanajua kazi unayoifanya, Mama unaweza"
0
April 22, 2020
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, amempongeza Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, kwa namna ambavyo ameamua kusimama na kupambana na ugonjwa wa Corona, na kumpongeza pia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kwa jinsi ambavyo alivyoamua kuwazuia watu kutoka mikoani kuja jijini humo ikiwa ni hatua ya kuzuia maambukizi kuenea kwa wingi.
Waziri Mkuu ameyabainisha hayo leo Aprili 22, 2020, wakati wa hotuba yake kwa viongozi wa dini na umma, wakati wa maandalizi ya maombi maalum ya Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya Corona.
"Nimshukuru sana Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, amefanya kazi kubwa sana na anaendelea kufanya kazi kubwa sana, yeye na Katibu Mkuu wake, Mganga Mkuu wa Serikali na Madaktari wetu wote, kazi mnayoifanya kama msingefanya hivyo tungekuwa kwenye hali mbaya, Watanzania wanajua kazi unayoifanya, Mama unaweza" amesema Waziri Mkuu.
Aidha wakati akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema,"Tunajua Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa Jiji lako ndiyo linaloongoza kwa maambukizi, tumeona pia jitihada zako zaidi za kusimamia, hata ulipowaambia kwamba jamani kwa watu wa nje sasa sio muhimu sana kwa wewe kuja na wale wa Dar es Salaam ukiona viongozi wanachokifanya huna haja ya kuzunguka tu mjini".
Katika kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, Waziri Mkuu amepiga marufuku wafanyabiashara wote wanaopandisha bei ya bidhaa na kwamba yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali dhidi yake.
Tags