MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa angalizo juu ya kuongezeka kwa migogoro ya familia na unyanyasaji wa kijinsia wakati huu wa maambukizi ya Virusi vya Corona.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kinachoendelea wakati huu ambapo shirika hilo na taasisi nyingine duniani zinapambana kuondoa virusi hivyo ambavyo vinachangia maambukizi ya Ugonjwa wa Covid-19, alisema kumekuwa na ongezeko la kesi nyingi kuhusu manyanyaso ya kijinsia hasa wa wanafamilia
“Wanawake wamekuwa wakinyanyaswa na kupigwa wakati huu ambapo wazazi na watoto wamekuwa wakitumia muda mwingi kuwa pamoja.
“Tatizo la msongo wa mawazo kutokana na hali ya kiuchumi ikiwemo kukosa fedha au kukosa kazi imesababisha kuwe na taharuki,” alisema Dr. Tedros.
Ameongeza kuwa ripoti ya wanawake kupigwa zimekuwa zikipokelewa kwa wingi, ambapo ameshauri serikali kuchukua hatua kuondoa hali hiyo.
Nchini Tunisia, kulikuwa na kesi sita za aina hiyo kwa mwezi uliopita ikiwa ni ongezeko la kesi nyingi tofauti na ilivyokuwa mwaka jana.
Hali hiyo ya wanawake kunyanyaswa na waume zao imeongezeka pia nchini Ufaransa hasa wakati huu ambapo kumekuwa na ukaribu wa wanafamilia wanaotakiwa kukaa ndani muda mwingi kukwepa maambukizi ya Corona.
“Tunasikitishwa na ripoti hizo tangu maambukizi yaanze kusambaa, tunaziomba mamlaka kwenye nchi zote kuwa na njia za kupunguza na kupambana na hali hiyo, hakuna kisingizio chochote cha kutesana kwenye familia,” alisema mkurugenzi huyo.