Na Paschal Dotto-MAELEZO
Serikali kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), leo imezindua rasmi filamu inayoitambulisha Tanzania ndani na nje ya nchi katika maeneo mbalimbali ya utalii ambayo inaendana na kauli mbiu ya Tanzania Isiyosahaulika “Tanzania Unforgettable” yenye kuitambulisha Tanzania duniani kote.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri Mwenye dhamana ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangala amesema kuwa Tanzania imeendelea kutangaza utalii pamoja na kuwepo kwa ugonjwa wa Covid-19, kwani, Rais Dkt.John Pombe Magufuli ameiongoza vyema nchi katika mapambano bila kuathiri sekta za kiuchumi ikiwemo Utalii.
“Namshukuru Mhe. Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuongoza vyema katika mapambano ya covid-19 bila kuathiri sekta za kiuchumi ikiwemo hii ya utalii, kwani kwa sasa tumefungua sekta hii, kama mnavyojua biashara ni ushindani atakeyewahi kufungua na kuweka misingi mizuri ya kuwahudumia wageni na wahudumu sekta ya utalii ndiye atakayepata faida zaidi, tumeamua kufungua utalii wetu na sasa anga letu lipo wazi kwa watalii”, Dkt.Kigwangala.
Amefafanua kuwa Tanzania imejipanga kuwahudumia vyema watalii watakao watawasili nchini na kuhakikisha kuwa wanaondoka salama ili wakifika katika nchi zao wapeleke habari njema kwamba Tanzania ni salama na watalii ambao walisita kuja waje bila woga.
Amebainisha kuwa Serikali imeamua kufungua sekta ya utalii kwa kufuata tahadhari zote zinazotolewa na mamlaka husika ikiwemo Wizara ya Afya ya Tanzania na Shirika la Afya Duniani (WHO), na kuwakaribisha watalii.
Katika uzinduzi huo, Waziri Kigwangala ametoa rai kwa Watanzania kuisambaza filamu hiyo kwenye mitandao yao ya kijamii ikiwemo Facebook, Twitter, Instgram, telegram na mitandao mingine, ili iweze kuwafikia walengwa kwa lengo la kutangaza Tanzania kiutalii katika soko la utalii la kimataifa.
“Hii ni video rasmi au filamu fupi kwa lengo la kuitambulisha nchi yetu kiutalii katika soko la utalii kimataifa, na hii imeendana sawa kabisa na kauli mbiu ya Tanzania Unforgettable kwa hiyo ninaomba Watanzania wenzangu tuisambaze kwenye mitandao yetu ya kijamii kwa maana imetafsiriwa katika lugha ya Kiswahili, Kingereza, Kifaransa, Kihispania, Kiisrael na Kichina”, Dkt. Kigwangala.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bi.Devotha Mdachi alisema kuwa Tanzania kwa sasa imejikita zaidi kutangaza vivutio vya utalii kupitia mitandao ya kijamii, kwa hiyo kuzinduliwa kwa filamu hiyo fupi kutawasaidia kuteka soko la ndani na nje ya nchi.
“Sisi Kama Bodi ya Utalii tumejikita zaidi kutangaza utalii kwa kutumia mitandao ya kijamii, kwani mpaka sasa tuna vipindi vinavyoruka mubashara kupitia mitandao yetu kwa mfano kipindi cha Serengeti safari show na kile kinachorushwa na Mamlaka ya Bonde la Ngorongoro, hizi ni moja ya njia za kutangaza utalii ndani na nje ya nchi”, Bi. Mdachi.
Ameongeza kuwa kupitia filamu hiyo fupi watalii watapata fursa ya kuona utamaduni na maeneo mbalimbali ya kuvutia na kuweza kuchagua sehemu sahihi ya kwenda kutembelea, amewataka Watanzania hasa watu maarufu kusambaza filamu hizo za dakika moja, dakika tatu, dakika saba na dakika 10 kwenye kurasa zao ili ziweze kufika mbali zaidi.
Mwisho.