Askari aliyemuokoa kichanga kwenye shimo la choo asimulia, aelezea maisha yake
0
May 26, 2020
Askari wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, Danis Minja ameeleza jinsi alivyofanikiwa kumuokoa mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja aliyekuwa ametupwa ndani ya shimo la choo Wilayani Ngara mkoani Kagera, pamoja na simulizi la maisha yake.
Minja amesema kuwa baada ya kusikia sauti ya mtoto, aliumia na aliwaambia wananchi waliokuwa wamefika katika eneo hilo kuwa anataka kuingia kwenye shimo hilo lenye urefu wa takribani futi 30. Kwa bahati nzuri, wananchi nao walionesha kumtia moyo zaidi.
“Niliwaambia wananchi, ninawakabidhi maisha yangu, na maisha ya mtoto yako mikononi mwangu, kwahiyo mnishushe kwa kamba ndani ya shimo, nitarudi na mtoto,” alisimulia.
Amesema kuwa wakati anaingia ndani ya shimo la choo hicho kilichokuwa kinatumika, alikuwa anamsikia mtoto akiwa bado analia, hali iliyompa matumaini zaidi.
“Kulikuwa na mbao ambazo zilitumika kujengea shimo la choo, kwa bahati nzuri mafundi walikuwa wameziacha, Mungu ni mkubwa. Hizo ndizo nilizotumia kuwa nazikanyaga, na nilimkuta mtoto amelalia mwili,” alisema.
“Yule mtoto alikuwa ametupwa nadhani kati ya majira ya saa tano na saa sita usiku, kwa sababu hiyo ndiyo inaweza kuwa mida ambayo aliyefanya kitendo hicho alijua watu wamelala,” ameongeza.
Minja amesema kuwa baada ya kumtoa mtoto huyo akiwa hai, alifurahi na kuwashukuru wananchi kwa kumlindia uhai wake aliokuwa amewakabidhi na hivyo kufanikisha yeye pia kuulinda uhai wa mtoto aliyemfuata ndani ya shimo hilo.
MamboSasa asimulia majambazi Saba walivyouawa na polisi
“Nawashukuru wananchi kwanza kwa kupiga simu ya bure ya kutoa taarifa kwa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, hii ndiyo kazi yetu na nchini kote tumekuwa tunafanya kazi nyingi za uokoaji kwa sababu tumepewa mafunzo mazuri,” alisema
Akizungumzia maisha yake, Minja amesema kuwa anaamini ujasiri wa kuchukua hatua hiyo ulitokana na malezi yake.
“Mimi nilikuwa mtundu kidogo nilipokuwa mdogo, sikuwa nakaa sana nyumbani, kwahiyo nilijikuta nalelewa na walezi karibu 20 na walinifundisha sana kuwa na hofu ya Mungu. Hata wazazi wangu waliolala sasa hivi, nawashukuru sana kwa malezi, nadhani yote haya yanatokana na malezi,” ameeleza.
Mei 22, 2020, Kamishina Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga alimpandisha cheo Minja kutoka Constable na kuwa Koplo.
Tags