Barack Obama Akemea Ubaguzi Nchini Marekani



Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama amehutubia kuhusu kifo cha raia mweusi wa Marekani George Floyd ambaye alipoteza maisha baada ya kukandamizwa kwa goti shingoni na afisa polisi nchini humo.

Obama amebaini kuwa wengi huko Marekani wako tayari kurudi katika maisha ya kawaida baada ya janga la covid-19 lakini kwamba inasikitisha na kuumiza kuona kuwa utofauti kati ya watu ni jambo la kawaida.

"Jambo hili halifai kuwa la kawaida nchini Marekani mwaka 2020. Haliwezi kuwa la kawaida," Obama, rais wa kwanza mweusi wa Marekani alisema katika taarifa hiyo.

"Ikiwa tunataka watoto wetu wakulie katika taifa lenye viwango vya juu zaidi ni lazima tuwe bora na tunaweza kuwa bora”,aliongeza rais huyo.

"Inatakiwa sana kwa maafisa wa Minnesota kuhakikisha kuwa kifo cha George Floyd kinachunguzwa vizuri na kwamba haki inapatikana. Lakini inatuhusu sisi sote, bila kujali kabila letu au tulipo – kufanya kazi kuunda kawaida mpya isiyokuwa na uonevu“.

Hata hivyo maneno ya Obama yanaonekana tofauti sana na yale ya rais wa sasa wa Marekani Donald Trump aliyeandika katika ukurasa wake wa twitter ya kuwa angetuma jeshi kushughulikia maandamano yanayoendelea juu ya kifo cha Mmarekani huyo na kusema yanatia dosari kumbukumbu ya George Floyd.

Maneno hayo ya Trump yamepingwa vikali na wengi ikidaiwa yanachochea ghasia.

Kifo cha George Floyd kinafanana sana na kile ya Eric Garner, ambaye alifariki mnamo mwaka 2014 baada ya kukamatwa na maafisa polisi mjini New York na kusema maneno kama aliyosema George ya kwamba "Siwezi kupumua."
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad