Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika (CDC) kimesema kwamba vifaa vya kupimia virusi vya corona nchini Tanzania havina shida yeyote. Leo Alhamisi, Mkuu wa Afrika CDC amewaambia waandishi wa habari kuwa ofisi yake inavijua vilivyo vipimo hivyo.
“Vipimo ambavyo Tanzania inatumia tunajua kwamba vinafanyakazi vizuri,” Dkt. John Nkengasong amesema hivyo katika mkutano na wanahabari wa njia ya mtandao.
Kauli hiyo ya Mkuu wa Africa CDC, inapingana na kauli ya Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli ambaye alisema huenda vipimo hivyo vikawa na matatizo.
Kituo hicho cha Africa CDC pamoja na wakfu wa Jack Ma, Shirika la msaada la bilionea wa China, lilisambaza vifaa hivyo, Nkengasong amesema na kuongeza kwamba vilidhinishwa na wanachojua ni kwamba vinafanya vizuri.
Kituo hicho kiko chini ya Umoja wa Afrika kina majukumu ya kuratibu mapambano dhidi ya mlipuko wa mangonjwa barani Afrika.
Rais Magufuli atilia mashaka ufanisi wa maabara, uchunguzi kufanyika
Siku ya Jumapili, Rais Magufuli alikihutubia taifa alitilia mashaka ufanisi wa vifaa vya kupima corona katika maabara kuu ya nchi hiyo.
Magufuli alieleza kuwa aliagiza sampuli za Wanyama na matunda kupewa majina ya binadamu na umri kisha kupelekwa ili zipimwe bila wataalamu wa maabara hiyo kujua na matokeo yakarudi kuwa baadhi ya sampuli hizo zimekutwa na maambukizi ya corona.
“…Lazima ugundue kuna mambo ya ajabu yanafanyika nchi hii. Ama wahusika wa maabara wamenunuliwa na mabeberu, ama hawana utaalamu jambo ambalo si kweli kwa kuwa maabara hii imetumika sana katika magonjwa mengine. Ama zile sampuli zinazoletwa maana vifaa vyote vinatoka nje, hivyo lazima kuna kitu fulani kinafanywa,” alisema Magufuli.
Magufuli alisema kutokana na taarifa hizo anaamini kuna watu ambao walipewa majibu yasiyo sahihi. “Lazima kuna watu wameambiwa positive lakini si wagonjwa wa corona, na inawezekana wengine wakafa kwa hofu.”