Dawa ambayo rais wa Marekani Donald Trump alisema anainywa inaongeza hatari ya kufa kwa wagonjwa wenye virusi vya corona, kulingana na utafiti wa jarida la Lancet.
Utafiti huo umeonesha kwamba hakuna faida yoyote ya kutibu wagonjwa na dawa hiyo ya kutibu malaria ya hydroxychloroquine.
Bwana Trump alisema alikuwa anakunywa dawa hiyo licha ya maafisa wa afya kuonywa kwamba inaweza kusababisha matatizo ya ugonjwa wa moyo.
Rais huyo amekuwa akipigia debe dawa hiyo mara kadhaa jambo linalokinzana na ushauri wa madaktari.
Dawa ya hydroxychloroquine ni salama sana kwa kutibu ugonjwa wa malaria, ugonjwa wa mapaku mekundu ngozini (lupus) na ugonjwa wa yabisi-kavu (arthritis) lakini hakuna majaribio ambayo yamependekezwa katika matumizi ya hydroxychloroquine kwa virusi vya corona.
Utafiti wa Lancet unajumuisha wagonjwa wa virusi vya coona 96,000 karibia 15,000 ambao walipewa dawa ya hydroxychloroquine - au wamepewa dawa yenye chloroquine - ama iwe peke yake au kwa kuchanganywa na viuavijasumu yaani antibaotiki.
Utafiti huo ulibaini kwamba wagonjwa walikuwa katika hatari ya kufa hospitalini na kupata matatizo ya moyo ikilinganishwa na wagonjwa wengine waliopata Covid-19.
Kiwango cha wanaokufa kwa makundi la waliotibiwa ni: asilimia 18 kwa dawa ya hydroxychloroquine; asilimia 16.4 kwa dawa ya chloroquine; na kundi lililodhibiti dawa hiyo ni aslimia 9.
Wale waliotibiwa kwa dawa ya hydroxychloroquine au chloroquine ambazo zilichanganywa na viuavijasumu yaani antibaotiki, kiwango cha waliokufa kilikuwa cha juu zaidi.
Watafiti wameonya kwamba dawa ya hydroxychloroquine isitumiwe isipokuwa tu kwa wanaofanyiwa najaribio hospitali.
Bwana Trump alisema yeye hajathibitishwa kuwa na ugonjwa wa Covid-19 na anakunywa dawa hiyo kwasababu anafikiria ina faida kubwa katika kukinga upatikanaji wa virusi vya corona.
Majaribio yanaendelea ya kutathmini ikiwa dawa hiyo ya kutibu malaria inaweza kuzuia ugonjwa wa Covid-19. zaidi ya wafanyakazi wa afya 40,000 kutoka Ulaya, Afrika, Asia na Amerika Kusini ambao wanatibu wagonjwa wa Covid-19 watapewa dawa hiyo kama sehemu ya majaribio.
Alipoulizwa kuhusu utafiti wa Jarida la Lancet, daktari mratibu wa jopo la kukabiliana na ugonjwa wa virusi vya corona katika Ikulu ya Marekani, Dr Deborah Birx alisema kuwa Shirika la Usimamizi wa Chakula na Dawa la Marekani limuweka wazi kuhusu wasiwasi wake katika utumiaji wa dawa hiyo ya kutibu malaria kama njia ya kuzuia virusi vya corona au kama matibabu.
Dkt. Marcos Espinal, mkurugenzi wa shirika liitwalo Pan American Health Organization ambalo ni sehemu ya Shirika la Afya Duniani - amesisitiza kwamba hakuna majaribio ya dawa hiyo hospitalini ambayo yamependekezwa katika utumiaji wa dawa ya hydroxychloroquine kwa virusi vya corona.