HATIMAYE dunia imeanza kuelewa falsafa na mitazamo ya Rais John Magufuli, katika kukabiliana na mambukizi ya virusi vya corona.
Miongoni mwa mitazamo ya Rais Magufuli tangu kuripotiwa kuingia kwa maambukizi ya virusi vya corona nchini katikati ya Machi, ni wananchi kutokuhofia ugonjwa huo, bali kuendelea na shughuli zao, huku wakichukua tahadhari zote ili kutopata maambukizi.
Awali, ilionekana kama baadhi ya mataifa na watu mbalimbali, walikuwa hawajaelewa vizuri mtazamo huo wa Rais Magufuli, lakini sasa ni dhahiri kutokana na mwenendo wa virusi vya corona kutokuonesha dalili ya kupatikana ufumbuzi wa karibuni, wameungana na Rais huyo wa Tanzania katika falsafa yake hiyo, likiwamo Shirika la Afya Duniani (WHO).
Rais Magufuli, tofauti na marais wengine duniani, alipinga mtazamo wa kuwafungia ndani watu na kusimamisha shughuli zote za kiuchumi kama njia ya kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya virusi vya corona.
Katika mtazamo unaonana na wa Rais Magufuli, WHO limesema jamii inapaswa kujifunza kuishi na corona huku shughuli nyingine zikiendelea, kwani hakuna dalili ya kumalizika hivi karibuni.
Shirika hilo linafananisha ugonjwa wa covid-19 unaosababishwa na virusi vya corona na ukimwi, ambao tangu uingie na kusambaa duniani, hadi leo jamii imejifunza kuishi nao na kuendelea na shughuli za kijamii na kiuchumi kama kawaida, licha ya kutopatikana kinga wala tiba mpaka sasa.
Mtazamo wa Magufuli Hivi karibuni, Rais Magufuli akizungumza na Watanzania, akiwa Chato, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo, huku wakichapa kazi kwa manufaa ili kuepuka athari kubwa zaidi za kijamii na kiuchumi, kwa kuwa virusi vya corona vinaweza visiishe haraka duniani.
“Inawezekana tukaishi na corona kwa muda mrefu kama tunavyoishi na magonjwa kama ukimwi, kifua kikuu, surua na magonjwa mengine. Ni muhimu sana tuendelee kufanya kazi kwa bidii kwa maendeleo ya taifa letu, wakati tukiendelea kuchukua tahadhari dhidi ya janga hili,” alisema Rais Magufuli.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli pamoja na kuwataka Watanzania kuondoa hofu juu ya ugonjwa huo, alisema hana mpango wa kufunga mipaka ya nchi wala kufunga maeneo ambayo yataonekana kuwa na maambukizi.
Hata hivyo, Rais Magufuli katika kuonesha serikali yake inachukua hatua kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari na kufuata masharti yote ya wataalamu wa afya kuhusu namna ya kujikinga na kuwakinga wengine wasipate maambukizi.
Mtazamo wa WHO
Siku chache baada ya kauli hiyo ya Rais Magufuli iliyozua gumzo katika jamii na mitandao, WHO ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na masuala ya afya duniani, limejitokeza hadharani na kueleza yaleyale aliyosema Rais Magufuli juu ya ugonjwa huo.
Akizungumza na kwenye mkutano wa waandishi wa habari kwa njia mtandao Mei 13, mwaka huu, Mkurugenzi wa Masuala ya Dharura wa WHO, Dk Mike Ryan, alisema ni muhimu dunia ikajiandaa na kujiweka tayari kwani janga halina dalili ya kuondoka hivi karibuni, hivyo inapaswa kutafuta njia za jinsi ya kuishi nalo huku shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi zikiendelea.
“Nafikiri wakati umefika tuwe wakweli, sidhani kama kuna mtu anaweza kutabiri kuwa ugonjwa huu utaisha hivi karibuni. Nafikiri hakuna ahadi wala tarehe katika hili. Ugonjwa huu unaweza kuwapo kwa muda mrefu, ni jambo linalowezekana,” alisema.
Dk Ryan alisema pamoja na uwezekano kuwa ugonjwa huo ukaendelea kuwapo, lakini jitihada za kuudhibiti zinaendelea, ikiwamo kwa chanjo zaidi ya 100 zinazofanyiwa utafiti kuhusu virusi vya corona.
Alisema pamoja na utafiti wa chanjo hizo, kuna magonjwa mengine kama vile tetekuwanga ambayo tangu yalipuke duniani bado hayajatokomezwa, licha ya kuwapo chanjo yake na kutahadharisha kuwa, hata kama chanjo ya covid-19 itapatikana, kudhibiti virusi vya corona kutahitajika juhudi kubwa.
Mtaalamu wa Majanga wa WHO, Maria van Kerkhove, aliwaambia waandishi wa habari kuwa, jamii inapaswa kuweka akilini kwamba, itachukua muda mrefu kuondokana na janga hilo. Baadhi ya wataalamu wanadai huenda janga hilo likachukua mwaka na zaidi kuondoka duniani.
Mataifa mengine Msimamo huo wa Rais Magufuli ikiwamo kutochukua hatua ya kuzuia watu kutoka ndani (lockdown) kama njia ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona, pia umeungwa mkono sehemu mbalimbali duniani.
Baadhi ya mataifa yaliyochukua hatua ya kuzuia watu kutoka ndani, yameanza kulegeza masharti, huku mengine yakifikiria kuondoa kabisa kutokana na athari yaliyopata ikiwamo kuzorota kwa shughuli za kijamii na kiuchumi, hivyo kuongeza ukali wa maisha kwa wananchi wao.
Nchini Afrika Kusini, juzi ilishuhudiwa mamia ya wananchi wakitoka ndani na kuingia barabarani ili kupaza sauti zao kuwa wanaumizwa na hatua hiyo, huku wakiwa hawana chakula wala mahitaji mengine muhimu na kuishinikiza serikali kuondoa zuio hilo pamoja na kuwapatia chakula.
Kauli za watendaji hao wa WHO na wataalamu wengine wa masuala ya afya duniani, zinaweka bayana kuwa, wakati mapambano dhidi ya virusi vya ukimwi yakiendelea, wakati huohuo shughuli za kiuchumi na kijamii zinapaswa kuendelea ili kuzuia kutokea janga jingine la kiuchumi na kijamii duniani.
Hatua inazochukua Tanzania Pamoja na kwamba Tanzania haijafunga maeneo yake (lockdown), imechukua hatua mbalimbali za kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona, ikiwamo kuunda kamati za kitaifa za kukabiliana na ugonjwa huo na kufunga shule na vyuo vyote nchini mpaka hapo hali itakapotengemaa.
Nyingine ni kutenga maeneo katika hospitali na mengine kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa wa corona na kutoa elimu kwa wananchi juu ya kujikinga kutopata virusi hivyo kwa kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya kama vile uvaaji wa barakoa, kupunguza safari zisizo za lazima, kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni, kukaa umbali wa mita moja ili kupunguza msongamano na kufika kituo cha afya mtu anapojihisi ana dalili za ugonjwa huo.