Ifahamu Zaka ni nini, aina zake na madhara ya kutokutoa




PAMOJA na kuwa zaka ni miongoni mwa nguzo tano za Kiislamu, lakini pia ni kiungo muhimu kati ya tabaka la matajiri na masikini, kwani utekelezaji wa nguzo hii unaleta ufanisi katika kuziba mwanya uliojitokeza kati ya matabaka mawili haya. 

Somo hili litasaidia kuwaelimisha Waislamu umuhimu wa zaka na jinsi ya kutekeleza nguzo hii muhimu. 

Maana ya zaka: 
Neno zaka maana yake ni baraka, utakaso, ziada na wema, mambo ambayo upatikanaji kwa kukusanywa viwango maalumu vya mali kutoka kwa wenye uwezo na kupewa watu wanaohitaji. Tofauti kubwa iliyopo kati ya zaka na sadaka ni kuwa, zaka ni tendo la lazima ambapo sadaka ni tendo la hiari (hisani). 

Hukumu ya kutoa zaka:  
Kutoa zaka ni jambo la lazima kwa Muislamu mwenye uwezo uliotajwa na sheria ya Kiislamu, Muislamu huyo akiacha kutoa zaka huwa ni mkosa anayestahili kuadhibiwa mbele ya Mungu.Mali ipasayo kutolewa zaka: 

Kitu chochote kile kinachomilikiwa na kutumika kwa maslahi ya binadamu ni mali ipasayo kutolewa zaka, hata hivyo, kuna mambo maalum yanayozingatiwa katika mali hiyo kama vile uzalishaji, kufikia lengo maalum na kupitiwa na muda wa mwaka. 

Aina za zaka: 
Kuna aina nyingi za zaka, zifuatazo ni baadhi ya aina hizo: 

Zaka ya Akiba: Mali yoyote iliyowekwa kama akiba mahali popote pale kwa lengo la kuihifadhi hutolewa zaka. 

Utaratibu wa zaka hii huwa kama ifuatavyo:


Iwe na thamani isiyopungua thamani ya gramu 85 za dhahabu safi (5,255,000/= Tsh). 
Kinachotolewa ni asilimia 2.5 ya mali yote. 
Iwe ina umri wa mwaka mmoja tokea imewekwa au kutolewa zaka. 



Zaka ya mifugo - Muislamu anayemiliki ng’ombe 30 anapaswa kutoa ng’ombe mmoja mwenye umri wa mwaka mmoja, na yule anayemiliki ng’ombe 40 atoe ng’ombe mwenye umri wa miaka miwili, utaratibu huu utumike katika kila kundi la ng’ombe 30 na ng’ombe 40, pia inaruhusika kutoa thamani ya ng’ombe waliotajwa. Kuhusu mbuzi na kondoo atatoa katika kila mbuzi au kondoo 100 mnyama mmoja anayehusika au thamani yake. Jambo muhimu ni kuzingatia muda wa mwaka moja tokea kunzishwa kwa ufugaji au kutolewa kwa zaka. 

Zaka ya mavuno - Kila kinachovunwa kutoka ardhini au baharini kinapaswa kutolewa zaka mradi tu mavuno hayo yana uzito usiopungua kilo 653 (gunia sita na nusu), kinachotolewa ni kilo 65.3 iwapo kilimo hakikutegemea gharama za kitaalamu, vinginevyo mkulima atapaswa kutoa kilo 33 tu kwa kila kilo 653 anazozivuna. 

Zaka ya biashara - Mali yoyote iliyotengezwa kwa ajili ya uzalishaji inapaswa kutolewa zaka mradi tu ina thamani isiyopungua shilingi 5,255,000 za Kitanzania. Kinachotolewa ni asilimia 20% (1/5) ya faida iliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja. 

Zaka ya machimbo - Kila kinachochimbwa ardhini au kukusanywa kutoka baharini miongoni mwa madini kinapaswa kutolewa zaka, kinachotolewa ni asilimia 20% ya thamani ya madini yaliyochimbwa au kukusanywa. 

Wanaostahiki kupewa zaka: 
Qur’an tukufu imetaja jamii nane za watu wanaostahiki kupewa zaka, nao ni hawa wafuatao: 

Mafukara: Hawa ni watu ambao hawamudu kupata mahitaji yao ya lazima kila siku. 

Masikini: Hawa ni watu ambao hawamudu kupata mahitaji yao ya lazima kwa uhakika.

Wenye madeni: Mtu au kikundi cha watu wenye madeni wanastahiki kupewa sehemu ya zaka ili waweze kulipa madeni yao. 

Watumishi wa zaka: Watu wanaotumika kukusanya na kusambaza zaka wapewe sehemu ya zaka hiyo kwa lengo la kuwafanya wasiwe na tamaa dhidi ya mali wanayoifanyia kazi. 

Harakati za ukombozi: Mtu au kikundi cha watu kinachotaka kujikomboa kutoka utumwani au kutawaliwa kimabavu wanastahiki kupewa sehemu ya zaka ili kufanikisha lengo lao. 

Wanaosilimu: Watu wanaoingia katika dini ya Kiislamu wanastahiki kupewa zaka ili waweze kulingana na maisha yao mapya ya Kiislamu. 

Wanaopatwa na maafa: Watu waliopatwa na maafa wanastahiki kupewa sehemu ya zaka ili waweze kufarijika dhidi ya maafa yaliyowapata. 

Wanaoendeleza dini ya Kiislamu: Kila anayeshughulika na miradi ya kuiendeleza dini ya Kiislamu kama vile kufundisha, kujenga Misikiti, shule na hospitali anastahiki kupewa zaka ili kufanikisha malengo hayo. 

Hitimisho: 
Wataalamu wengi wa Kiislamu wameelezea umuhimu wa kuwa na chombo maalum cha kukusanya na kusambaza zaka badala ya kila tajiri kujitolea zaka kwa utaratibu wake binafsi, hali hii haipendezi wala haileti ufanisi mzuri katika kuuendeleza Uislamu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad