Indhari ya WHO; Huenda Corona ikaua Watu 190,000 Barani Afrika


Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya kuwa, yumkini ugonjwa wa Covid-19 (corona) ukaua watu baina ya 83,000 na 190,000 katika nchi za Afrika ndani ya miezi michache ijayo, iwapo maradhi hayo hayatadhibitiwa.

Indhari hiyo ilitolewa jana Alkhamisi na Matshidiso Moeti, Mkurugenzi Mkuu wa WHO barani Afrika ambaye anasisitiza kuwa, iwapo hatua za makusudi za kuudhibiti ugonjwa huo hazitachukuliwa, basi corona itasalia kuwa sehemu ya maisha ya nchi za Afrika kwa miaka kadhaa ijayo.

Amesema WHO ina wasi wasi kuwa yumkini Waafrika kati ya milioni 29 na 44 wataambukizwa virusi vya corona ndani ya mwaka wa kwanza wa kuenea ugonjwa huo barani Afrika, iwapo hatua za tahadhari zitaendelea kupuuzwa.

Afisa huyo mwandamizi wa WHO barani Afrika ameeleza bayana kuwa, takriban madaktari 1,000 barani Afrika wamekumbwa na virusi vya corona, katika hali ambayo nchi nyingi za bara hilo zina uhaba wa matabibu na maafisa wengine wa afya.

Shirika la Afya Duniani limesema nchi ndogo na maskini za Afrika pamoja na Afrika Kusini, Algeria na Cameroon zinatazamiwa kuwa waathirika wakuu wa mlipuko wa corona barani Afrika karibuni hivi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad