Iran: Serikali ya Marekani inaunga Mkono Ubaguzi wa Rangi
0
May 30, 2020
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameashiria mauaji dhidi ya Wamarekani weusi yanayofanywa na polisi ya nchi hiyo na kusisitiza kwamba, serikali ya Marekani inaunga mkono ubaguzi wa rangi.
Sayyid Abbas Mousavi ameyasema hayo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter na kuongeza kuwa, mauaji ya kutisha na yaliyotekelezwa na polisi kirahisi na bila wasiwasi wowote dhidi ya George Floyd Mmarekani mweusi aliyeuawa na polisi mweupe, ni dhihirisho la ubaguzi wa rangi wa kimfumo na kujiona bora watu weupe, unaopongezwa na kufadhiliwa na watawala wa sasa wa Marekani.
Hii ni katika hali ambayo Jumatano iliyopita Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran pia iliandika kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba miaka 6 baada ya polisi ya Marekani kumkandamiza na kumuua raia mwingine mweusi wa Marekani kwa jina la Eric Garner, aliyekuwa akiomba msaada kwa kusema: "siwezi kupumua", Mmarekani mwingine mwenye asili ya Afrika, George Floyd ameuawa kwa kutumika mbinu ile ile ya kukandamiziwa chini hadi akakata roho.
Aidha Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imebainisha kwamba inaonekana kwamba ukandamizaji na ukatili wa polisi wa Marekani dhidi ya Wamarekani weusi hautambui mpaka wowote na kama ilivyo kawaida, jibu la serikali ya Marekani kwa wanaotaka kutekelezwa uadilifu, huwa ni ukandamizaji na utumiaji mabavu mkubwa zaidi. Kwa mujibu wa ripoti, katika kipindi cha miezi minne ya mwanzo wa mwaka huu, zaidi ya raia 200 wamepoteza maisha kutokana na ukandamizaji wa polisi wa Marekani. Kwa kawaida mahakama za Marekani huwa zinawaachilia huru polisi wanaotenda jinai dhidi ya Wamarekani weusi au kuwapa adhabu hafifu ikilinganishwa na makosa waliyofanya
Tags