SIMBA wapo tayari kwa utaratibu wowote utakaotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikiwemo suala la upimaji wa afya ili kujiridhisha kuwa wachezaji wao wote akiwemo Meddie Kagere na Aishi Manula hawana maambukizi ya virusi vya Corona kabla ya kuendelea kwa michuano ya Ligi Kuu Bara.
Kauli hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ikiwa ni siku chache baada ya Serikali kuruhusu michezo kuendelea Juni Mosi, mwaka huu.Senzo alisema: “Tunahesh-imu maamuzi yaliyotolewa na Serikali, tumejiandaa na tuko tayari kwa ajili ya kuendeleza kampeni yetu ya kusaka ub-ingwa wa Ligi Kuu Bara.
“Kwa sasa tunasubiri TFF na Bodi ya Ligi watupe utaratibu wa namna gani tutarejea uwanjani na tutatoa ushirikiano wa kutosha hata ikihitajika kupima afya za wachezaji wetu.
”Hivi karibuni, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harrison Mwakyembe, alisema wamepanga baada ya ligi kurudi, vitumike viwanja vya Taifa, Uhuru na Azam Complex jijini Dar kwa mechi za Ligi Kuu Bara pekee, huku Ligi Daraja la Kwanza na Ligi Daraja la Pili zitumie CCM Kirumba na Nyamagana jijini Mwanza.