KENYA: Karantini Zageuzwa Madanguro


MAAFISA wa serikali Kaunti ya Nyamira wanasema baadhi ya watu wanaozuiliwa karantini kwa kushukiwa kuwa na virusi vya corona wamebadilisha vituo hivyo kuwa madanguro ya kufanyia mapenzi.

Kulingana na Kamishna wa hiyo, Bw Amos Mariba na Waziri wa Afya wa kaunti hiyo Douglas Bosire, baadhi ya watu walio karantini wamekuwa wakishiriki vitendo vya ngono katika vituo hivyo na kujiweka katika hatari zaidi ya kupata virusi hivyo kwa kukiuka agizo la kutokaribiana.

Maafisa wa serikali sasa wameapa kuchukua hatua ikizingatiwa kuwa tabia hiyo inaweza kusambaza virusi hivyo.

Watu 95 wamewekwa karantini ya lazima kwa kukiuka kanuni za kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona kaunti ya Nyamira.

Miongoni mwa vituo wanamozuiliwa ni shule ya wavulana ya Nyambaria iliyoko kaunti ndogo ya Manga, shule ya upili ya Nyakongo iliyoko Masaba Kaskazini, shule ya upili ya Menyenya iliyoko Borabu, shule ya wasichana ya Kebabe iliyoko Nyamira Kaskazini na shule ya wasichana ya Sironga inayopatikana Nyamira Kusini.

Bw Mariba alisema serikali haitaweka vifaa vya kujikinga wakati wa kufanya mapenzi katika vituo vya karantini.

“Haya ni maeneo yaliyotengwa na hatutaruhusu yeyote kupeleka kondomu huko. Hatukubali tabia ya ukahaba katika jamii,” alisema.
“Wale wanaoingia karantini, wanafaa kuzingatia kanuni zilizowekwa na pia kutuarifu maovu yanayofanyika huko,” alisema Bw Bosire.

Bw Mariba alisema wale wanaokiuka kanuni za karantini watazuiliwa kwa muda mrefu katika vituo hivyo.

Kamishna huyo wa kaunti alikuwa akizungumza katika makao makuu ya kaunti ya Nyamira ambapo kamati ya eneo hilo ya kukabiliana na janga la corona ilipokea misaada kutoka kwa taasisi tofauti.

Katika kaunti ya Bomet, serikali imewaweka karantini watu wanne waliotoroka kutoka kaunti ya Nairobi. Watu hao walikamatwa umma ulipowaripoti kwa maafisa wa serikali. Kamishna wa kaunti hiyo Geoffrey Omoding alisema kwamba washukiwa hao wanatoka eneobunge la Chepalungu.

Watu hao watashtakiwa baada ya kukamilisha karantini.

Katika kaunti ya Kisumu, Gavana Anyang Nyong’o alisema watu 157 wamekaguliwa. Jumatatu, watu 87 waliopimwa korona hawakupatikana na virusi hivyo. Alisema serikali yake iliwapa mafunzo wahudumu wa afya na kuunda kamati vijijini vinavyoshirikisha machifu na wanachama wa nyumba kumi kukabiliana na corona.

Katika kaunti ya Migori, watu 25 wanaoshukiwa kutangamana na wagonjwa wawili wa corona, wamewekwa karantini. Miongoni mwa watu hao ni wanabodaboda na watu 23 wa familia moja kutoka eneo la Kuria Mashariki.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad