CORONA bado ipo na inaua, ni vizuri wapendanao na jamii nzima kwa ujumla ikazidi kuchukua tahadhari ambazo zinatolewa kwenye vyombo mbalimbali vya habari. Kubwa zaidi, ni vizuri kubaki nyumbani kama huna shughuli ya lazima inayokufanya utoke.
Tukirejea kwenye maisha yetu ya mahusiano, mada kama inavyojieleza hapo juu. Suala la kuchepuka kwenye ulimwengu wa sasa, limekuwa kama vile ni jambo la kawaida. Si wapenzi, wachumba hata wanandoa, wote wanachepuka.
Japo lipo kwenye maeneo yote hayo niliyoainisha, lakini kwa wanandoa ni tatizo kubwa zaidi. Wachumba au wapenzi wanapoanza urafiki, huwa mara nyingi wanaheshimiana. Hawana sana sababu ya kuchepuka.
Hata kama wanachepuka, ni nadra sana lakini wanapofikia kwenye ndoa, ndipo tatizo linapokuwa sugu. Kwa utafiti mdogo nilioufanya, wanandoa ndio wanaoongoza zaidi kwa kuchepuka sasa hivi kuliko hata wachumba.
Lakini hapa lazima tujiulize ni kwa nini wanachepuka? Sababu hasa ni nini? Japo kila mmoja anaweza kuwa na sababu zake, lakini miongoni mwa sababu zinazopewa uzito ni pamoja na watu kuzoeana. Watu wanafikia wakati sasa, kila mmoja anamuona mwenzake wa kawaida.
Sasa ili kupata radha mpya, ndipo anapoona bora achepuke ajaribu radha mpya. Bahati mbaya sana, anapoanza mwanandoa mmoja, ni rahisi sana na mwenzake kufuatia mkondo huo. Hii inatokana na yule aliyeanza kusaliti, huwa inafika mahali ananogewa.
Hata ikitokea ameshtukiwa na mwenzake, akaonywa vipi, anakuwa mzito kuacha. Anaendelea kuchepuka tena, anaponogewa anaweza kuwa na michepuko zaidi ya mmoja. Leo anakuwa na huyu, kesho na yule kesho kutwa anabadilisha mwingine.
Mwenzake anapopambana kumrejesha kwenye mstari, anajishusha kwa muda lakini baada ya muda anaendelea. Hapa sasa ndipo mwenza wake naye anapojikuta ameshawishika kirahisi naye kuchepuka. Anachepuka sababu, mwenzake kanogewa.
Mwenzake hasikii wala haoni. Anachepuka hadi inafika mahali nyumbani hatoi huduma stahiki. Mambo yote anayamalizia kwa michepuko. Akirudi nyumbani ni kulala na kutimiza majukumu mengine ya kifamilia kama kuhudumia watoto, tena wengine wanasahau mpaka watoto!
Ndio maana siku hizi tunashuhudia wanandoa wa kiume wakichepuka sana lakini pia hata wa kike nao wanachepuka. Ukipeleleza kwa makini, utagundua kuna mmoja alianza, mwenzake naye akafuatia. Mambo yanakuwa ni kuchepuka kwa kwenda mbele.
Eti kila mmoja anafanya kwa siri. Anachohakikisha tu ni mwenzake asijue ndani. Hiyo imekuwa ndio fasheni ya sasa. Mtu anajitahidi kutoa huduma ya ndani kwa mazoea, lakini anajua furaha yake ipo kwa ‘kamchepuko’ kake huko nje.
Ndugu zangu, pamoja na kwamba mbinu hii inawasaidia wengi kuishi kwa amani, lakini lazima tuelewe kwamba, hii mbinu si sahihi. Ni hatari kwa mustakabali wa ndoa yenu. Ni vizuri kuheshimu misingi ya ndoa, kila mtu akampa heshima mwenzake.
Kama kuna kitu kimepungua, ni vizuri mkaelezana na mkakiweka sawa ili kama mlivyoanza safari pamoja, basi muendelee pamoja mpaka pale kifo kitakapowatenganisha. Usifikiri kufanya kwa siri ni ujanja, ni ujinga tu ambao siku ukibainika unaweza kuondoa kabisa maana ya ndoa yenu.
Ya nini kuiweka rehani ndoa yenu? Simama na mkeo au mumeo. Acha tamaa, utajiona mjanja leo lakini unaweza pia kuleta maradhi ndani ya nyumba.
Tukutane wiki ijayo. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii; Instagram&Facebook: Erick Evarist, Twitter: ENangale.
Je, ingekuwa wewe ungefanyaje? Tuma maoni yako kupitia namba 0768 811 595