Na Amiri kilagalila,Njombe
Madiwani watatu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA wilayani Makete mkoani Njombe,wamehama chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi CCM.
Madiwani hao ni miongoni mwa madiwani kutoka kata saba zinazoongozwa na CHADEMA,hali inayofanya Chama hicho kubakiwa na kata nne katika kata ishirini na tatu zilizopo wilayani Makete huku kata nyingine zikiongozwa na CCM.
Akizungumza wakati akiwapokea madiwani hao,katibu wa siasa na uenezi mkoa wa Njombe Ndg,Erasto Ngole amesema madiwani aliowapokea ni pamoja na Asifiwe Luvanda aliyekuwa diwani wa kata ya Iwawa,Betrece Kyando aliyekuwa diwani wa viti maalum kutoka tarafa ya Lupalilo na Efati Mbogela Mwipelele aliyekuwa diwani wa kata ya Ipelele.
Ngole amewataka madiwani hao kuto kuogopa kusema ukweli ndani ya Chama cha Mapinduzi kwa kuwa Chama hicho chini ya Rais Dkt,John Pombe Magufuli ndivyo kinavyotaka kwa kuzingatia taratibu,kanuni na sheria kupitia katiba.
“Nyinyi mnaokuja usiogope kusema ukweli,moja iwe moja na mbili iwe mbili,ndivyo CCM ya sasa inavyotaka na ndivyo mwenyekiti wetu Magufuli alivyo,kwa hiyo njooni huku mje mshauri,mtembee na sisi, na zile tabia zako ulizokuwa nazo CHADEMA ambazo wananchi wanazipenda endelea nazo ili wananchi kwa tabia ile ile wakaendelee kuipenda CCM”Alisema Erasto Ngole.
Merry Mkoka ni katibu wa Jumuiya ya wanawake UWT mkoa wa Njombe,amesema anaamini madiwani hao wamevutiwa na utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi pamoja na ushirikiano mzuri baina ya Chama na serikali.
“Nimezungumza hivyo kwasababu ya ushirikiano mzuri na upendo mzuri baina ya Chama na Serikali ndio maana nimeona DC wa Makete yuko hapa leo”alisema Merry Mkoka
Naye Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Ona Sukunala Nkwama amesema madiwani hao hawajawahi kukasfu wala kukebehi Chama cha Mapinduzi huku wakitekeleza miradi mingi kwenye kata zao,hivyo amewahakikishia ushirikiano wa hali ya juu ndani ya CCM.
“Niwahakikishie Chama kitakuwa na ninyi na mtapata ushirikiano wa hali ya juu wala hamtajutia maamuzi yenu hayo”
Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Makete Ndg,Ignatio Mtawa amesema madiwani hao amekuwa nao zaidi ya miaka minne kama mwenyekiti wao ndani ya baraza la madiwani,anawafahamu vizuri kwa kuwa walikuwa ni wapinzani wa kweli kwa kujua wapi wapinge na kuunga mkono.
“Naomba nizungumze kwa wapinzani wote Tanzania,hawa madiwani watatu kwenye baraza langu mimi niliwahesabu kuwa ni wapinzani wa kweli kwa kuwa walikuwa wanajua wapi wapinge na wapi waunge mkono,kwa kweli kenye sehemu ya kuunga mkono waliunga na kwenye sehemu ya kupinga walipinga sasa yalipoisha ya kupinga ndio maana wamechukuwa uamuzi huu,hawa walikuwa wanajenga hoja kwenye baraza vizuri sana na hakuna hoja yao niliyowahi kuona ni ya kipuuzi”alisema Mtawa
Aidha mkuu wa wilaya ya Makete Bi,Veronika Kessy amesema madiwani hao walikuwa mstari wa mbele kutekeleza Ilani katika maeneo yao bila msuguano wowote,hivyo yuko tayari kuendelea kuwaongezea ulinzi hasa katika kipindi hiki kwao.
“Mimi naona Madiwani hawa waliorudi Chama cha Mapinduzi wote hawa ni CCM kwasabubu walikuwa mstari wa mbele katika kutekeleza Ilani kwenye maeneo yao,kwa hiyo nasema hawa ni wenzetu walikuwa tu wamechepuka kwa kwenda upande ule na leo wamerudi kutokana na heshima ya Mh.Rais”alisema Veronika Kessy
Betrece Kyando, Asifiwe Luvanda na Efati Mbogela Mwipelele ni madiwani waliohama Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA,wamesema wamehama chama hicho bila shinikizo la mtu yeyote hivyo wanaamini wapo watakao umia na watakao furahi,huku Betrece Kyando akiwahakikishia Chama cha Mapinduzi kwenda kufanya kazi pasipo kusimama kwenye maslahi ya mtu.
“Siku zote sijawahi simama kwenye maslahi ya mtu kwa kuwa imani yangu ni kwamba Makete ni namba moja,na sitakuwa tayari kuto kufanya yale yaliyonipasa ndani ya chama eti kwasababu ya maslahi ya mtu fulani Mwenezi ukiskia nilikaidi ujue nilikuwa kinyume na anayenituma lakini kama anachonituma ni sahihi kwa maslahi ya umma nitafanya sawa sawa na nilivyotumwa”alisema Betrece.