Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali hoja za pingamizi za awali za mfanyabiashara James Rugemarila na wenzake wawili ikiwemo kutaka kuachiwa huru.
Mshitakiwa mwingine ni Habinder Seth na Joseph Makandege ambao wanakabiliwa na mashitaka 12 yakiwemo ya utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Serikali zaidi ya U.S.D Mil. 22,198,544.60 na Sh.Bil 309,461,300,158.27.
Uamuzi huo umetolewa mahakamani hapo na Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shaid. Mshtakiwa wa kwanza James Rugemarila Februari 29, 2020 aliwasilisha hoja ya kumtaka Mkurugezi wa Mashtaka (DPP) atoe kibali cha kumwachia huru na ikiwa atashindwa kufanya hivyo basi Mahakama hiyo imuondoe katika kesi hiyo huku Makandege ambaye ni mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo akiwasilisha hoja zake Machi 26, 2020 zilizodai kuwepo mapungufu katika hati ya mashtaka yanayomkabili
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon amedai mahakamani hapo kuwa shauri hilo lililetwa kwa ajili ya kusikiliza uamuzi mdogo wa mapingamizi ya awali ya mshtakiwa wa kwanza na wa tatu katika kesi hiyo.
Uamuzi huo Hakimu Shaidi amesema kuwa mahakama yake haiwezi kutoa amri kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wala kumwachia mshtakiwa kwa sababu haina mamlaka ya kufanya hivyo na wenye mamlaka ya kufanya hivyo ni Mahakama Kuu kwa mujibu wa sheria na kibali cha DPP.
Rugemarila na Seth walifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Juni 19, 2017.