Mapinduzi ya Muziki Bongo… Kiba, Harmo Waungana!




KWA mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva, hii ni zaidi ya good news! Habari ikifikie kwamba, mafundi wawili; Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ na Rajab Abdul ‘Harmonize’ wana jambo lao ambalo liko jikoni, litakapokapokamilika dunia itaelewa nini maana ya muziki mzuri.

Taarifa ambazo Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limezinyaka kutoka pande zote mbili zinaeleza kuwa, wawili hao, kila mmoja alikuwa na shauku ya kufanya kazi ya pamoja na tayari sasa wameshafikia mahali pazuri kuweza kushirikiana kwa ukaribu.

NI HISTORIA

Endapo mambo yatakwenda kama yalivyopangwa, itakuwa ni histori ya mapinduzi ya muziki wa Bongo Fleva, Harmonize au Harmo anakwenda kufanya kazi na Kiba ambaye inaaminika ni hasimu mkubwa wa bosi wake wa zamani, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’.

Kikizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA, chanzo makini kilisema kwamba, Harmo na Kiba wameshafanya makubaliano mazuri ya kushirikiana katika ‘project’ ambayo bado hawaamua kuitangaza, lakini itakuwa inahusika na kazi.

“Ni project ambayo itakuwa na nyimbo nyingi kulingana na wao wenyewe watakavyoona inafaa, ni wakati mzuri wa mashabiki wa Kiba na wale wa Harmo kufurahia muziki mzuri na historia nyingine inakwenda kuandikwa,” kilisema chanzo hicho.

WATAENDELEA KUFANYA KAZI ZA KIPEKEE

Chanzo hicho kilisema kuwa, haimaanishi kwamba Kiba na Harmo hawatakuwa wakifanya kazi za peke yao, bali watakuwa wakikutana kwenye project hiyo kulingana na jinsi ambavyo uongozi wao utakuwa umekubaliana.

“Watakuwa wanakutana studio, wanafanya nyimbo kisha kila mmoja anaendelea na biashara zake nyingine maana wao kila mmoja ana uongozi wake,” kilisema chanzo hicho.

LENGO NI KUMWANGUSHA MONDI?

Chanzo hicho kilisema kuwa, lengo la Kiba na Harmo kushirikiana si kushindana na Diamond au Mondi ila ni kufanya muziki mzuri maana wanaamini wakiunganisha nguvu zao, muziki wao utaweza kufika mbali zaidi.

“Wao hawashindani na mtu bali wameamua kufanya muziki wao. Mashindano hawayapi nafasi. Kama unavyomfuatilia Kiba amekuwa akifanya muziki mzuri miaka mingi, Harmo naye ana utawala wake, ana timu yake kubwa tu ya ushindi na anafanya vizuri,” kilisema chanzo hicho.

MENEJA WA KIBA

Gazeti la IJUMAA WIKIENDA lilizungumza na mmoja wa mameneja wa Kiba, Aidan Seif ambapo alipoulizwa kuhusu muunganiko wa wawili hao, alisema Kiba kufanya ngoma na mtu yeyote kwao siyo tatizo ilimradi tu wakubaliane.

“Tusubiri, tu hakuna kitakachoshindikana kikubwa ni makubaliano,” alisema Aidan.

MENEJA WA HARMO ANASEMAJE?

Akizungumza na Gazeti la IJUMAA WIKIENDA kuhusu ishu hiyo, meneja wa Harmo, Beauty Mmary ‘Mjerumani’ naye aliwataka mashabiki wa pande zote mbili wakae mkao wa kula kwani ni jambo la heri.

“Kwanza mashabiki wasubiri ikitoka wataiona, nitazungumza baada ya hiyo kolabo, lakini Harmo ni mwanamuziki mzuri na Kiba pia ni mwanamuziki mzuri, wakiona wanaweza kuungana na kufanya biashara watafanya na itakwenda public (kwa umma) na tutaizungumzia wakati huo, lakini kwa sasa tuache kwanza,” alisema.

TUJIKUMBUSHE

Kwa muda mrefu, Harmonize amekuwa akisisitiza kuwa, yupo tayari kufanya kazi na msanii yeyote ndani na nje ya nchi hata Kiba ambaye ni mpinzani mkubwa wa aliyekuwa na bosi wake wa zamani wa Lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB), Diamond Platnumz.

“Mimi ni msanii, naweza kufanya kolabo na msanii yeyote sina shida wala tatizo na msanii yeyote ndiyo maana nasema Konde Boy is for everybody na nadhani kitu kinachoinua muziki wa Afrika Magharibi ni kolabo, silaha pekee itakayoinua muziki wetu ni kufanya kolabo sisi kwa sisi,” alisisitiza Harmonize katika moja ya intavyuu zake hivi karibuni.

Project hii ikikamilika, inatarajiwa kuwa gumzo la aina yake kwa sababu watu wengi wanaamini Kiba na Harmo, wote ni mahasimu wa Mondi hivyo kutengeneza himaya yao yenye nguvu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad