Marekani Kuipa Tanzania Bilioni 5.6 za Ziada Kusaidia Kupambana na Corona
0
May 23, 2020
Marekani imetangaza kuwa kupitia Shirika lake la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) itaongeza kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 2.4 (Takriban Shilingi za Kitanzania bilioni 5.6), ikiwa ni msaada kwa sekta ya afya nchini Tanzania ambapo msaada huu unalenga kuimarisha uwezo wa maabara na upimaji wa kimaabara, kusaidia jitihada za utoaji taarifa, miradi ya maji na usafi wa mazingira, kuzuia na kudhibiti maambukizi, kutoa elimu ya afya kwa umma na miradi mingine.
Fedha hizi ni nyongeza ya msaada wa Dola za Kimarekani milioni 1 unaolenga kusaidia mapambano dhidi ya janga la COVID-19 uliotolewa hivi karibuni na kufanya kiasi kipya cha fedha zilizotolewa kwa Tanzania ili kukabiliana na janga hili kufikia Dola za Kimarekani milioni 3.4.
Isitoshe, kiasi kingine cha Dola za Kimarekani milioni 1.9 zimebadilishwa matumizi na kuelekezwa kwenye mapambano dhidi ya janga hili.
Hii inafanya jumla ya fedha zote zilizotolewa na Marekani katika kukabiliana na COVID-19 nchini Tanzania hadi hivi sasa kufikia Dola za Kimarekani milioni 5.3 (Sawa na Shilingi za Kitanzania bilioni 12.2).
Taarifa hiyo imeongea kuwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita Marekani imewekeza zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 7.5 kwa maendeleo ya Tanzania huku karibu Dola za Kimarekani bilioni 4.9 zikielekezwa kwenye sekta ya afya pekee ambapo toka mwaka 2009 Serikali ya Marekani imetoa zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 100 kusaidia miradi ya afya na takriban Dola za Kimarekani bilioni 70 kama msaada wa kibinadamu duniani kote.
Imeeleza pia kuwa, Serikali ya Marekani inaendelea kuwa mfadhili mkubwa zaidi duniani wa miradi ya afya na shughuli za kibinadamu zinazolenga maendeleo ya muda mrefu na jitihada za washirika wake kujijengea uwezo na kuchukua hatua za dharura wakati wa majanga. Aidha tunaongoza duniani katika utoaji wa misaada ya kibinadamu na kiafya katika kukabiliana na janga la COVID-19.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, Marekani inaendelea kuonyesha uongozi katika jitihada za kimataifa za kukabiliana na janga la COVID-19, Watu wa Marekani wametoa zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 10 zitakazosaidia jitihada za kimataifa za kukabiliana na COVID-19
Tags