Matukio ya Watu Kuanguka Mitaani na Kufa, Madaktari Wanena Mazito



KUTOKANA na wimbi la watu wenye umri chini ya miaka 50 kuanguka na kupata kiharusi na wanapopimwa hubainika kuwa na maambukizi ya Virusi vya Corona, Watanzania wameshauriwa kufanya mazoezi kwa wingi na kula vyakula vyenye kinga.

Hatua hiyo imekuja baada ya watu hao kubainika kuwa na Virusi vya Corona bila kuwa na dalili zozote kama vile mafua makali, homa, kikohozi, kupiga chafya au vidonda kooni.



Tangu maambukizi ya Corona yabishe hodi nchini Tanzania Machi 16, mwaka huu na idadi ya maambukizi kuongezeka kufikia 480 (Mei 9, mwaka huu), kumekuwa na taarifa, video na picha mnato zinazoonesha sura za watu waliofariki dunia ghafla katika maeneo mbalimbali ikiwamo Kariakoo, hotelini na wengine hospitali.

Licha ya kwamba taarifa hizo zinadaiwa kuhusisha vifo hivyo vya ghafla na maambukizi ya Corona, Gazeti la IJUMAA WIKIENDA limezungumza na baadhi ya madaktari ili kupata ufafanuzi wa kina kuhusiana na maambukizi ya Corona pamoja kiharusi.

Akizungumza na IJUMAA WIKIENDA hili, Dk Sadick Sizya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili alisema ni dhahiri upo uhusiano kati ya Virusi vya Corona na kiharusi ambacho kinasababisha watu kuanguka ghafla na kufariki dunia.

Akizidi kufafanua, Dk Sizya alisema kinachotokea ni kwamba Virusi vya Corona vinapoingia katika mwili wa binadamu huingia moja kwa moja kwenye mzunguko wa damu.

“Katika mwili wa binadamu kuna seli nyekundu za damu, seli nyeupe na seli sahani. Hawa Corona wanaingia katika seli nyekundu yenye madini kama vile madini ya chuma na protini.

“Gamba la wale Virusi wa Corona lina protini pia, sasa wanapoingia yale madini ya chuma kwenye damu hutoka na mwili kuzalisha damu kwa wingi, kumbe wale virusi wameudanganya mwili kuwa damu imepungua, hali hiyo husababisha damu kuzidi na nyingine kuganda kwenye mishipa ya damu.

“Katika mfumo wote huo mwili hujibu kwa kuanzisha damu kuganda (coagulator effects) au kuvimba (inflammatory effects) ambapo mambo hayo mawili yakitokea katika mishipa ya damu ya binadamu, mishipa ya damu huziba ghafla na kupata hali ambayo kitaalam huitwa Large Vessels Occlusion au kuziba kwa mishipa mikubwa ya damu na kusababisha mgonjwa kuanguka na kupata kiharusi na hata kupoteza uhai wake mara moja.

“Hii ndiyo imekuwa sababu kubwa sana ya vijana wengi kuanguka ghafla na kufa. Vijana chini ya miaka 50 wanaanguka na kufariki ghafla maiti zikipimwa zinakutwa na maambukizi ya Virusi vya Corona, ingawa hawakuwa na dalili hata moja.

“Wanapopimwa wamekutwa na maambukizi ya Corona, lakini hawakuwahi kupatwa na homa, kikohozi ama mafua makali,” alisema.

NINI KIFANYIKE?

Ripoti iliyotolewa Agosti mwaka jana na Jarida la African Journal of Emergency Medicine ilibainisha kuwa asilimia 20 ya wagonjwa wanapatwa na kiharusi hususan wenye umri kuanzia miaka 43 hadi 70.

Wakijadili ripoti hiyo katika siku ya kiharusi duniani, daktari bingwa wa mishipa ya fahamu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Patience Njenje alisema hospitali hiyo hupokea wagonjwa watano kwa siku wenye tatizo la kiharusi.


Alisema tatizo la kiharusi lilikuwa ni tatizo la watu wa nchi za Ulaya, lakini sasa limehamia Afrika baada ya Waafrika kuiga mfumo wa maisha ya wazungu.

Hoja hiyo iliungwa mkono pia na Dk Sizya ambaye alishauri kuwa ni vema watu kufanya mazoezi mara kwa mara ili kupunguza uzito na kurahisisha mishipa ya damu kupitisha damu kwa urahisi.

“Kwa sababu watu wanakula malimao na matunda mengine yanayoongeza vitamin mbalimbali ikiwamo C, lakini wamesahau kuwa ili kuongeza kinga pia tunahitaji kufanya mazoezi na kuwa na uzito sahihi. Watu wana uzito mkubwa unaominya mishipa ya damu na kusababisha kiharusi ambacho kina uhusiano na Corona,” alisema.

Aidha, daktari huyo amefafanua kwamba pale hali hiyo inapojitokeza dawa pekee inayoweza kutolewa ni ya kuyeyusha damu (blood thinners) kama Junior Aspirin au dawa za kupunguza uvimbe ziitwazo Steroids.

“Dawa hizi hazitakiwi kutolewa bila ushauri wa daktari, watu wasinywe kwa mazoea sababu ni hatari kutumia bila ushauri wa daktari kwani aspirin ina madhara kwa wenye vidonda vya tumbo,” alisema.

Aidha, Dk Walter Kweka kutoka Hospitali ya TMJ jijini Dar, naye alifafanua mtindo wa watu kutofanya mazoezi mara kwa mara ni mojawapo ya kutokea kwa vifo vya ghafla hasa kwa vijana chini ya miaka 50.

“Kwa sababu ndiyo wenye uzito mkubwa, ni mara chache kukuta wazee wenye uzito mkubwa. Hasa ikizingatiwa kwamba vijana wana misuli ikilinganishwa na wazee ambao misuli yao husinyaa. Hivyo kuna umuhimu sana wa kufanya mazoezi ili kuzuia kutopatwa na tatizo hilo la damu kuganda kwenye mishipa,” alisema.

KIHARUSI TANZANIA

Tatizo hilo la kiharusi kwa upande wa Tanzania linashika namba sita kwa kusababisha vifo nchini.

Magonjwa ya kifua kikuu na magonjwa ya homa ya mapafu na mafua ndiyo yanayoongoza kwa kusababisha vifo.

STORI: MWANDISHI WETU, DAR

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad