Misiba ya Watu Maarufu iliyoibua Gumzo la Corona Tanzania


Ndani ya kipindi cha mwezi mmoja uliopita watu kadhaa maarufu nchini Tanzania kuanzia Jaji Mkuu mstaafu, waziri hadi viongozi wa dini wamefariki.

Japo sababu ya vifo vyao kutosemwa ama kuwa ni tofauti na corona kumekuwa na mjadala wa namna vilivyotokea ghafla na kwa kuongozana na pia juu ya hatua za tahadhari ambazo zimekuwa zikichukuliwa kwenye mazishi yao.

Mchungaji Getrude Lwakatare, ambaye alikuwa mchungaji mkuu wa Kanisa la Mlima wa Moto jijini Dar es Salaam na Mbunge wa Viti Maalumu nchini Tanzania aliaga dunia Aprili 20 jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa familia yake, kifo chake kilisababishwa na shinikizo la damu na matatizo ya moyo. Siku moja baadaye, Spika wa Bunge Job Ndugai akatangaza kuwa mazishi yake yatasimamiwa na serikali na kuwa yatahudhuriwa na watu wasiozidi 10.

Japo haikusemwa kuwa ni corona, ila ni utaratibu wa serikali kuongoza mazishi ya watu waliofariki kwa virusi hivyo na kuzuia idadi ya waombolezaji kwa uchache unaowezekana.

Siku chache baadae, Aprili 25 aliyewahi kuwa mbunge wa kisiwa cha Mafia Abdulkarim Shah alifariki dunia katika hospitali moja jijini Dar es Salaam na kuzikwa asubuhi ya siku iliyofuata na watu wachache.

Aprili 27, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara (Kusini mwa Tanzania) Evod Mmanda alifariki dunia. Akithibitisha taarifa za kifo chake Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Sulemani Jafo alisema Mmanda alilazwa hospitali kwa siku mbili kabla kufikwa na mauti na alikuwa akikabiliwa na "changamoto za upumuaji."

Mazishi ya Mmanda yalifanyika siku iliyofuatia yakisimamiwa na serikali huku ndugu zake 10 tu wakiruhusiwa kushiriki.

Tarehe 27 Aprili pia ilishuhudia majaji wawili wastaafu nchini humo wakifariki, Jaji Ali Haji Pandu ambaye aliwahi kuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar na moja ya waasisi wa chama cha CUF na Jaji Mussa Kwikama ambaye alikuwa kiongozi mwandamizi wa chama cha ACT Wazalendo.

Siku hiyohiyo Naibu Meya wa Manispaa ya Morogoro Isihaka Sengo alifariki dunia hospitalini. Siku iliyofuata mazishi yake ambayo yalikuwa yamepangwa na familia yalisitishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Morogoro akisema marehemu alionesha dalili za virusi vya corona, na baadae mazishi yake yalisimamiwa na serikali na kuhudhuriwa na ndugu wachache.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad