JINA la kwenye pasipoti ni David Adedeji Adeleke lakini lile la kuburudisha ni Davido. Ni bonge moja la mwandishi wa ngoma kali, mtayarishaji wa muziki na mwimbaji wa levo za juu barani Afrika.
Davido ni mtoto wa mfanyabiashara bilionea wa Kinigeria, Dk Deji Adeleke. Huyu mshikaji amezaliwa Novemba 21, 1992 kwenye familia ya Dk Deji na Bi Vero Adeleke ndani ya Atlanta, Georgia nchini Marekani. Baadaye familia hiyo ilirejea nyumbani jijini Lagos, Nigeria.
Akiwa na umri wa miaka 13, Davido alianza kujifunza utayarishaji wa muziki kupitia studio tofauti na baadaye kujiunga na kundi la muziki la shuleni alipokuwa ‘high school’.
Baadaye alianza kufanya kazi na wasanii chipukizi wa wakati huo nchini Nigeria kama Dammy Krane, NPZ na wengine kibao wa miondoko ya Afro- Pop na Afro-Beat.
Albam yake ya Dami Duro aliyoitoa Novemba 2011, ndiyo iliyomfanya kuwa mwanamuziki anayependwa zaidi nchini Nigeria. Hadi mwishoni mwa mwaka jana, alikuwa Balozi (brand ambassador) wa Kampuni ya Mawasiliano ya MTN ya Nigeria.
Tunapomzungumzia Davido yupo kwenye levo za wanamuziki kama P-Square, D’Banj, Wizkid, Don Jazzy, Tekno na wengine kimapato kupitia mikataba mikubwa ya kibiashara (endorsement).
Albam ya Dami Duro ilikuwa na ngoma matata sita za Back When, Ekuro, Overseas, All of You, Gbon Gbon na Feel Alright.
Baada ya albam hiyo, Davido aliendelea kutisha kimuziki akifanya kolabo na kila dizaini ya mastaa kama Wizkid, Ice Prince, 2face, Skales, Olamide na wengine wengi.
Ngoma nyingine zilizomuweka juu Davido ni Assurance, Flora My Flawa, Wonder Woman, The Sound, Gobe, Dodo, Coolest Kid in Africa, Blow My Mind na nyinginezo ambazo zimekuwa zikifanya poa kwenye platform mbalimbali za mitandao ya kijamii, lakini hazikuweza kuvunja rekodi iliyowekwa na ngoma yake nyingine kali ya Fall.
Bado midundo na melodi za ngoma hiyo zinasikika kwenye chati mbalimbali ndani na nje ya Bara la Afrika tangu ilipoachiwa Juni 2, 2017.
Ngoma hiyo imeandikwa na Davido chini ya Producer Kiddominant au Kiddo.
Ngoma hiyo ilitoka miezi mitano tu baada ya ngoma yake nyingine ya If ambayo ilitoka Februari 17, 2017.
Ngoma hizo zilitoka kwa mfumo wa back to back kwani If haikuachwa itambae sana, kwani ilifuatiwa na Fall.
Wakati If ikijikusanyia watazamaji zaidi ya milioni 105 hadi sasa, Fall inakimbiza vibaya mno ikiwa imetazamwa na zaidi ya watazamaji milioni 165 hadi sasa kwenye Mtandao wa YouTube.
Hakuna ngoma ya mwana-muziki yeyote barani Afrika yenye watazamaji au rekodi kama hiyo ya kibabe.
Fall ni ngoma ambayo imeweka rekodi ya kipekee barani Afrika. Ndiyo inayoshika namba moja kwa kutazamwa zaidi si ndani ya Afrika tu, bali hata nje ya Afrika.
Kwa mujibu wa mwanamuziki wa Bongo Fleva, Vanessa Mdee ‘Vee-Money’ bado ile midundo na melodi za Fall zinasikika kwenye spika za makorido ya mall kubwa za Supermarket za Walmart kule LA (Los Angeles), Marekani.
Taarifa ikufikie kuwa, Fall imewahi kutisha kwenye Chati za Billboard kule Marekani.
Februari 2019, Fall iliingia kwenye kumi bora ya nyimbo zilizojikusanyia mashabiki wengi kwa kusikilizwa zaidi kule New York, Marekani.
Kama hiyo haitoshi, Machi 2020, Fall ilifikisha wasikilizaji milioni 40 kwenye Mtandao wa Spotify. Hakuna ngoma nyingine yoyote kwenye bara hili iliyofikisha idadi hiyo ya usikilizwaji.
Fall imewahi kumnyima usingizi staa wa Hip Hop wa Marekani, Busta Rhymes ambaye aliamua kuifanyia remix.
Rapa mwingine mkali wa Marekani, Cardi B naye ilimzuzua kiasi cha kuifanyia remix ngoma hiyo akiwa na Davido.
Kibongobongo, wapo jamaa zangu kibao ambao wamekuwa wakijitahidi kufanya poa kupitia ngoma zao kali na kujikusanyia watazamaji wa kutosha kwenye YouTube, lakini bado wana deni kubwa kuifikia rekodi hiyo ya Davido.
MONDI
Ngoma zake zimekuwa zikifanya vizuri YouTube kwa kutazamwa na watazamaji wengi. Ngoma yake ya Yope Remix na Innoss’B wa Kongo, imetazamwa mara zaidi ya milioni 84 ndani ya miezi saba kwenye YouTube.
Nyingine ni Nana aliyofanya na Mr Flavour wa Nigeria iliyotoka miaka minne iliyopita ambayo hadi sasa imejikusanyia watazamaji milioni 61. Nana inafuatiwa na Inama aliyomshirikisha Fally Ipupa kutoka Kongo ambayo imetazamwa mara milioni 56 ndani ya muda wa miezi kumi.
Nyingine ni African Beauty aliyomshirikisha Omarion yenye watazamaji milioni 47. Bado hadi sasa Mondi hana ngoma iliyotazamwa zaidi ya mara milioni 100.
HARMO
Ngoma zake kali zilifanya vizuri tangu akiwa chini ya Wasafi Classic Baby (WCB) ni pamoja na Kwangaru akiwa na Mondi ambayo imetazamwa mara zaidi ya milioni 61 kwenye YouTube ndani ya miaka miwili.
Nyingine ni Bado aliyomshirikisha Mondi ambayo imetazamwa zaidi ya mara milioni 25 ndani ya miaka minne. Bado hajafikia spidi ya Davido.
KIBA
Ngoma za Mfalme Kiba zilizofanya vizuri, Mwana ambayo imekuwa na watazamaji zaidi ya milioni 25 kwenye YouTube kwa muda wa miaka mitano.
Kwa sasa Kiba anakimbiza na Kichupa cha Dodo kwenye YouTube ambacho kina zaidi ya watazamaji milioni 3 ndani ya wiki mbili.
VANNY BOY
Kichwa kingine cha Wasafi kinakimbiza kwenye YouTube. Kichupa kama Tetema akishirikiana na Mondi, kimetazamwa mara zaidi ya milioni 41 kwa muda wa zaidi ya mwaka mmoja.
Miss Buza ni ngoma nyingine ambayo bado inaendelea kuwa na watazamaji wengi na hadi sasa imetazamwa zaidi ya mara milioni 3 kwa muda wa mwezi mmoja. Bado naye anapanga foleni kwa Davido.