Msimamo usioyumbishwa! Hiyo ndiyo picha aliyoitengeneza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwenye vyombo vya habari vya kimataifa, baada ya kueleza waziwazi mashaka yake juu ya mashine zinazotumika kupima sampuli za wagonjwa wa Corona.
Akizungumza kutokea Chato, mkoani Geita wakati wa hafla fupi ya kumwapisha Waziri wa katiba na Sheria, Mwigulu Nchemba, Rais Magufuli alieleza wasiwasi wake juu ya mashine hizo huku akitolea mfano jinsi sampuli kutoka kwenye papai, mbuzi na ndege aina ya kware zilivyotoa majibu kuonesha kwamba wahusika wana maambukizi ya Corona.
Kauli yake hiyo, imeripotiwa na vyombo vikubwa vya habari duniani, kuanzia televisheni za BBC, DW, CBS, VOA, AL Jazeera, Sky News, CNN na kadhalika, huku magazeti ya New York Times, Financial Times, Daily Mail, The Guardian, Times of India yakiipa uzito habari kuhusu alichokizungumza.
Shirika la Habari la Reuters, nalo pia limeiripoti habari hiyo kwa ukubwa katika vyombo vyake mbalimbali, na kuzidi kuifanya hotuba ya Magufuli kuwa mjadala unaoumiza vichwa vya wanasayansi duniani kote kuhusu ubora na ufanisi wa vifaa vinavyotumika kupima Corona duniani kote.
Vyombo hivyo vya kimataifa, ambavyo mara kwa mara hushutumiwa kuandika habari mbaya pekee kutoka barani Afrika, safari hii vimejikuta vikiizungumzia habari ya hotuba ya Rais Magufuli kwa uzuri kwa sababu alichokibaini kuhusu ufanisi wa mashine hizo, kinahitaji mjadala mpana wa kitaalamu.
Katika hafla ya kumwapisha Mwigulu, Rais Magufuli alieleza jinsi sampuli kadhaa zilivyopelekwa kwenye Maabara Kuu ya Taifa, bila ya wataalamu wa maabara hiyo kujua kuwa si za binadamu, kisha majibu yakatoka kwamba sampuli hizo zilizokuwa zimepewa majina ya binadamu, zilikuwa na Corona wakati kiuhalisia zilikuwa ni sampuli za papai, ndege kwale pamoja na mbuzi.
“…Papai lile lipo halijafa linaiva tu. Mbuzi yule yupo tu hajafa, fenesi lile lipo tu labda lije kuoza… kwa hiyo natoa wito kwa Watanzania msiwe na hofu…mbona mafua yamekuwepo lakini haya ni makali, nayo yatapita…,” alisema Rais Magufuli katika hotuba yake aliyoitoa katika hafla hiyo.
Vyombo hivyo vimeendelea kumnukuu Rais Magufuli akisema: “…Lazima ugundue kuna mambo ya ajabu yanafanyika nchi hii. Ama wahusika wa maabara wamenunuliwa na mabeberu, ama hawana utaalamu jambo ambalo si kweli kwa kuwa maabara hii imetumika sana katika magonjwa mengine. Ama zile sampuli zinazoletwa maana vifaa vyote vinatoka nje, hivyo lazima kuna kitu fulani kinafanywa.”
Rais Magufuli, ambaye hadi sasa anatajwa kuwa rais kutoka nchi za Kiafrika anayeheshimika duniani kote kutokana na kuwa na misimamo isiyoyumbishwa, alisema kutokana na taarifa hizo anaamini kuna watu ambao walipewa majibu yasiyo sahihi kwamba wameambukizwa Corona wakati si kweli na kuongeza pengine kuna waliopoteza maisha kwa sababu ya hofu.
Rais Magufuli pia alivishutumu vyombo vya habari vya kimataifa kwa namna vinavyoripoti kuhusu janga hilo nchini Tanzania licha ya kuwa vyombo hivyo vipo katika maeneo ambayo yameathirika na ugonjwa huo kuliko hata Tanzania