Ndege Nyingine isiyo na Rubani ya Uturuki yatunguliwa Katika Anga ya Libya
0
May 10, 2020
Wanamgambo wa jenerali muasi Khalifa Haftar wamesema kuwa wametungua ndege moja isiyo na rubani ya Uturuki kusini mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Gazeti la al Rai al Yaum limeripoti habari hiyo na kusema kuwa, wanamgambo wanaojiita Jeshi la Taifa la Libya wanaoongozwa na jenerali muasi Khalifa Haftar, usiku wa kuamkia leo Jumapili wametangaza kuwa wametungua droni ya Uturuki aina ya "Bayraktar TB2" katika eneo la Ain Zara kwenye viunga vya kusini mwa Tripoli, mji mkuu wa Libya.
Mara chungu nzima wanamgambo wa Jenerali Khalifa Haftar wamekuwa wakitangaza kutungua ndege zisizo na rubani za Uturuki katika anga ya Libya.
Uturuki ambayo inaiunga mkono Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa yenye makao yake mjini Tripli, Libya, imetuma wanajeshi wake nchini humo kwenda kuilinda serikali hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu Fayez al Sarraj kukabiliana na mashambulizi ya wanamgambo wa jenerali muasi, Khalifa Haftar.
Khalifa Haftar anaongoza serikali ya mashariki mwa Libya na anaungwa mkono na Saudi Arabia, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) na baadhi ya nchi za Magharibi.
Mwezi Aprili 2019, jenerali huyo muasi alianzisha mashambulizi makubwa ya pande zote dhidi ya mji wa Tripoli kwa tamaa ya kuuteka haraka na kuivunja Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa iliyoundwa na Umoja wa Mataifa, lakini ndoto yake hiyo imeshindwa kutimia kutokana na muqawama na kusimama imara serikali hiyo ya Tripoli.
Tags