Nyani Waiba Damu za Wagonjwa wa Corona Kutoka Maabara


Kundi la nyani limeiba sampuli ya damu za watu waliopimwa virusi vipya vya corona (covid-19) katika hospitali ya umma, wilayani Meerut, Jimbo la Uttar Pradesh, nchini India.

Mkuu wa Taasisi ya Lala Lajpat Rai Memorial Medical College and Hospital, amekaririwa na vyombo vya habari nchini humo akieleza kuwa sampuli hizo zilikuwa damu pekee na sio sampuli zinazochukuliwa kutoka puani na kooni kwa mtu anayetakiwa kupimwa covid-19. Lakini, alithibitisha kuwa damu hizo zilichukuliwa kutoka kwa watu watatu waliobainika kuwa na maambukizi ya virusi vya corona, na kwamba zilikuwa zinaenda kufanyiwa vipimo vingine.

Kwa mujibu wa CNN, tukio hilo lilitokea Alhamisi wiki hii, wakati mhudumu msaidizi wa maabara inayopima covid-19 alikuwa amebeba damu hiyo ya sampuli.

Dkt. Dheeraj Baliyan, ambaye pia ni msimamizi wa taasisi hiyo, aliiambia CNN kuwa nyani walimvamia mhudumu huyo wa maabara na kumnyang’anya box lililokuwa na sampuli hizo tatu.

Alieleza kuwa nyani hao walikwea miti na kukimbia na sampuli hizo kwa muda. Alisema walizitupa baada ya kuchana vifungashio vilivyokuwa na damu hizo.

Dkt. Baliyan  alifafanua kuwa kwa bahati nzuri hakuna mtu aliyeguswa na damu hizo zilizomwagika, na kwamba walifanya usafi kwa kutumia vitakasa mikono (sanitizers) katika eneo lote husika.

Hadi sasa, India imeripoti visa zaidi ya 182,000 vya corona, wagonjwa 86,984 wakiwa wamepona na vifo 5,164.

ATCL yasafirisha abiria 200 waliokwama nchini

Rwanda yaripoti kifo cha kwanza cha mgonjwa wa corona

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad