WAZIRI wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Profesa Palamagamba John Kabudi amesema leo akiongea na wanahabari katika Ukumbi Wa Mikutano Wa Kimataifa Wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam ameyasema haya:
“Nilikwenda Madagascar na ndege ya Rais kupokea zawadi maalum ya dawa kutoka nchini Madagascar. Rais Magufuli aliniruhusu niende na wataalam…na tulipofika kule walikuwa na mkutano wa saa nne wa kuzungumza na wenzao kuhusiana na dawa hii,”
“Tumerudi kutoka Madagascar jana usiku ila hatujaja na dawa ya kuanza kugawa leo, tumekuja na dawa za kuanza utafiti na uchambuzi maabara, nimepokea simu nyingi, meseji WhatsApp Watu wanataka niwagaie, jamani sina dawa, sijaja na chupa za dawa”
“Madagascar wameijaribu wakajiridhisha kwamba ni salama ndio maana wanaitumia lakini sisi lazima tuifanyie utafiti na tujiridhishe kuwa inafaa,Ndege ya Rais haiwezi kuja na mzigo wa kutosha kugaiwa kwa Watanzania wote,Nchi yoyote ikituita kwamba ina dawa tutaenda kuchukua”
“Niwaeleze watanzania…hatujaja na dawa kwa ajili ya kuwagawa watanzania …dawa hizi ni kwa ajili ya utafiti na uchambuzi. Utafiti ukikamilika na tukiridhika tutazigawa kwa watanzania,”
“Tumepewa chupa mbili tu ambazo zitasaidia pale wataalamu watakapochanganya dawa na kufanya utafiti na uchambuzi ili waone kama wamepatia. Tumepewa box3 za dawa itakayotumika kama tiba na Box 8 za dawa itakayotumika kama kinga,”
“Kile sio kikombe cha Babu, hatukwenda kuchukua kikombe cha Babu ile ni dawa ya kisayansi, ndio maana tumeenda na Wataalamu, mimi peke yangu kwakuwa ni Waziri nimepata bahati ya kugonga ile dawa, ila zile chupa tumekuja nazo 2 tu za kusaidia utafiti, hatuna dawa kugawa”
“Watu waendelee kuchukua tahadhari hata kama tunaona hizi juhudi za uwepo wa matumaini ya dawa, lakini tuchukue tahadhari, hata sisi kwenye Ndege ya Rais tulikaa mbalimbali na tumevaa mask”