May 5, 2020 by Global Publishers
WIZARA ya Afya imetangaza visa vipya vinane vya #COVID-19 nchini humo na idadi ya maambukizi imefikia 97. Sita kati ya wagonjwa hao ni madereva malori waliogundulika baada ya sampuli 2,061 kufanyiwa vipimo na wawili ni wananchi wa kawaida.
Rais Yoweri Museveni amesema tahadhari zilizowekwa awali zitaendelea kuwepo kwa siku 14 wakati baadhi ya sekta muhimu zikiwemo kilimo na uzalishaji zimeruhusiwa kutoa huduma na kutakiwa kufuata taratibu za mamlaka ikiwa ni pamoja na kuvaa barakoa.
Aidha, Museveni amewataka wananfunzi kuendelea kusalia majumbani hata kama ni mwaka mzima na kwamba shule hazitafunguliwa mpaka corona iishe kabisa nchini humo.
“Shule nyingi ni za kutwa chache za bweni lakini zina wanafunzi wengi, ni hatari kuruhusu wanafunzi warudi shule/vyuoni, acha watoto waendelee kula bata nyumbani wakati tunapambana na corona, hata wakikosa muhula wote au mwaka mzima ni bora kuliko kukosa uhai wao,” amesema Rais Museveni.
Licha ya ongezeko la maambukizi nchini humo, Rais Museveni amesema usafirishaji mizigo lazima uendelee kwani kupiga marufuku kunaweza kusababisha madhara kiuchumi kwa sababu wanaleta bidhaa muhimu.
Taratibu mbalimbali zimetolewa kwa madereva ikiwemo kupima #CoronaVirus kwa hiari ili kudhibiti maambukizi zaidi. Madereva hao pia wametakiwa kuepuka kusimama bila sababu za msingi kwenye maeneo ya watu.