MDAU maarufu wa masuala ya soka nchini na mchezaji wa zamani wa Simba SC, Ismail Aden Rage, amekana kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Tabora kwa tuhuma za kugawa rushwa na kuanza kampeni za kugombea ubunge kabla ya muda kinyume na sheria.
Rage amefunguka hayo wakati akizungumza na Front Page ya +255 Global Radio, leo Jumanne, Mei 26, 2020 ikiwa ni siku moja tangu Takukuru walipotoa taarifa ya kumshikilia kwa mahojiano kiongozi huyo wa zamani wa Simba SC na TFF.
“Ni kwamba mimi Takukuru hawajanikuta mahala popote natoa hela wala hawajinukuta popote na wanachama wa CCM. Takukuru walinifuata nilikuwa nafuturu, wakaniambia alhaji wewe malizia futari halafu tutazungumza.
“Nikawauliza iweje tangu tangu tarehe 16 mje kunihoji leo siku 73 zimepita? Kwanza mimi sijatangaza nia mpaka sasa wala sijaamua kwamba nitagombea au sitagombea. Napima upepo kwanza. Mimi kwetu Tabora na bahati mbaya mbunge ambaye yupo sasa hatokei Tabora sasa nahisi labda ana hofu na mimi.
“Ilipofika asubuhi saa mbili wakaniachia, wakaniambia shehe nenda upo huru na tukikuhitaji tutakuita. Nikawaambia mimi naishi Dar es Salaam, naweza kwenda? Wakaniambia hata nje ya nchi nenda. Nawapongeza Takukuru maana wakisikia taarifa wana wajibu wa kufuatilia, wamenichukua nyumbani kwangu sivyo kama mitandao inavyosema, ooh nimedakwaaaa!” alisema.