Serikali Yawataka madereva wa malori nchini kuchukuwa tahadhari dhidi ya Virusi vya Corona



Na WAMJW – Dar es Salaa
Serikali imewataka madereva wa malori nchini kuchukuwa tahadhari dhidi ya Virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Corona (COVID-19) hii ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanakula vyakula ambavyo vitalinda kinga zao za mwili.

Rai hiyo imetolewa hivi karibuni na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (WAMJW) Ummy Mwalimu  wakati akizungumza na baadhi ya madereva wa kampuni mbalimbali za malori zinazosafirisha  mizigo nje ya nchi waliofika katika maabara ya  Taifa ya afya ya jamii iliyoko mabibo jijini Dar es Salam kwa ajili ya kupima kama wana maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Corona au la.

Waziri Ummy alisema ugonjwa wa Corona bado upo ingawa maambukizi yamepungua jambo la muhimu ni kwa wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa afya hii ikiwa ni pamoja na kuepuka mikusanyiko isiyokuwa  ya lazima, kunawa mikono kwa sabuni na  maji safi yanayotiririka, kuvaa barakoa pia kukaa umbali wa zaidi ya mita moja kati ya mtu na mtu.

“Nimefurahi sana kuwaona mko hapa kwa ajili ya kupima virusi vya Corona kama mtakutwa hamna maambukizi ya ugonjwa huu mjitahidi kula matunda yakiwemo machungwa, mananasi, malimao,  mboga za majani na  tangawizi hii itawasaidia kinga zenu za mwili kuwa juu. Pia muwapo safarini mnapopata nafasi msisahau kupiga nyungu,’’, alisema waziri Ummy.

Naye  Kaimu Mkurugenzi wa maabara ya Taifa ya afya ya jamii Ambele Mwafulango  alisema pamoja na kupima vipimo vya wagonjwa wengine  kwa upande wa madereva walioko jijini Dar es Salaam kwa siku wanawapima madereva 200 kwa madereva walioko mikoani kuna utaratibu maalum wa kuchukuliwa  sampuli ambazo zinatumwa Dar es Salaam kwa ajili ya vipimo.

Majibu ya vipimo hivyo yanatoka  baada ya  masaa 48 kama madereva hao  watakutwa hawana maambukzi watapewa vyeti ambavyo vinatumika kwa siku 14  hii itawasaidia kwenda kupeleka mizigo nje ya nchi bila ya kupimwa tena katika nchi wanazokwenda.

Mwafulango alisema kabla madereva hao hawajafanyiwa vipimo vya Corona wanapimwa joto la mwili na wale ambao watakutwa na joto la juu la mwili watapewa huduma ya haraka zaidi ukilinganisha na wale ambao joto lao la mwili liko sawa.

“Madereva ambao tunawakuta hawana maambukizi ya ugonjwa wa Corona tunawapa elimu ya kujikinga na ugonjwa huu wanapokuwa safarini siku zote ’’.

“Katika maabara hii ya Mabibo tuna mashine mpya tano ambazo ndani ya masaa 24 zinapima vipimo 1800 hii imetufanya kupima vipimo vingi zaidi ukilinganisha na  ilivyokuwa katika maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii iliyoko ofisi za NIMR jijini Dar es Salaam ambapo tulikuwa na mashine mbili ambazo zilikuwa zinapima vipimo 300 hadi 400 jambo ambalo lilikuwa linachelewesha utendaji wetu wa kazi,’’, alisema Mwafulango.

Serikali imetenga utaratibu malum kwa ajili ya madereva wa malori wanaosafirisha mizigo nje ya nchi ambao wanafanyiwa vipimo vya ugonjwa wa Corona  kabla ya kusafiri ili kuhakikisha hawana maambukizi na kuwaepusha kupata usumbufu ambao utajitokeza wanapokuwa safarini.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad