Simba Waitenda Yanga Kitu Mbaya




SI unajua Yanga ndiyo ambao wapo katika mstari wa mbele kuhakikisha wanawachukua mastraika wawili wa Rayon Sports, Michael Sarpong raia wa Ghana na Mrundi, Jules Ulimwengu? Sasa wapinzani wao Simba wamewatenda kitu mbaya.

 

Kabla hatujaenda mbali, nikukumbushe tu kuwa, GSM ambao ni wadhamini wa Yanga, wameshafanya mazungumzo na wachezaji hao, kilichobaki ni kuwapa mikataba tu wawe mali yao rasmi.

 

Sasa kitu mbaya ambacho Simba wamekifanya ni kuanza kuwafuatilia kwa ukaribu wachezaji hao wawili kwa ajili ya kutibua mambo na kuwashusha kikosini kwao.Hiyo imekuja baada ya Simba kupewa mchongo kuwa wawili hao wanatisha wakiwa wanacheza pamoja uwanjani na kama wakiwaruhusu kuvaa uzi wa wapinzani wao Yanga, basi msimu ujao watapata tabu sana kuwania mataji na yote yataenda Jangwani.



Mchongo huo Simba wamepewa baada ya kumtumia kiungo Kakule Mighuen Fabrice ambaye alikuja Simba msimu uliopita kwa ajili ya kufanya mazungumzo lakini dili lake lilishindikana, kisha kiungo huyo raia wa DR Congo kurejea katika klabu yake ya Rayon Sports ya Rwanda alipo hadi sasa.

 

Baada ya Simba kukabidhiwa mchongo huo, mabosi wa timu hiyo wameamua kumpa kazi aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Crescentius Magori ambaye alifanikisha klabu hiyo kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara kwa ajili ya kuwachunguza kisha kuwapa ripoti kamili.

 

Habari ambazo Spoti Xtra, limezipata ni kuwa nje ya Magori kukabidhiwa asimamie zoezi hilo, pia wamempa kazi maalum straika wao Meddie Kagere aliye Rwanda kuhakikisha anatuma taarifa za wachezaji hao kabla ya kuwapa mikataba.

 

“Kilichopo kwa sasa ni kuwa Simba wamepewa mchongo mzima juu ya Sarpong na Ulimwengu namna ambavyo wanaelewana wakiwa uwanjani ambapo wameonywa kwamba kama wakiwaruhusu waende Yanga basi watakuwa wameumia.

 

“Baada ya kupewa taarifa hizo Simba wamempa kazi maalum Magori ya kuhakikisha anafanya tathmini na kupata kila kitu kuhusiana na wachezaji hao wawili kwa sababu yeye ana mawasiliano mazuri na Kakule.

 

“Kuonyesha kwamba wamedhamiria kuwatibulia Yanga kwa washambuliaji hao pia Simba wamempa kazi maalum Kagere ya kuhakikisha kwamba naye anakuwa sehemu ya watu ambao wanapata taarifa za wachezaji hao kwa ajili ya kufanikisha dili linakamilika,” kilimaliza chanzo hicho.

 

Wakala wa Ulimwengu, Roro Stratton alisema: “Kuna ofa mbili kutoka timu kubwa Tanzania tumezipata, ni kweli Simba wameonesha nia ya kumtaka Ulimwengu na nitakutana nao siku yoyote kuanzia wiki ijayo.

 

”TAMKO LA GSMKlabu ya Yanga kupitia wadhamini wao Kampuni ya GSM, wamesema hawana tatizo lolote kuhusiana na hilo licha ya kwamba tayari wameshafanya mazungumzo na kukukubaliana vitu kadhaa.

 

Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, amesema: “Licha ya kuwa hatujawapa mikataba wachezaji hao, lakini ukweli ni kwamba hakuna ambaye anaweza kukataa kuja kwetu kwa sababu tulishafanya nao mazungumzo na kukubaliana vitu vya kimkataba.”

STORI: MUSA MATEJA NA SAID ALLY, Dar es Salaam

KICHUYA Afunguka MAZITO Yaliyomkuta UARABUNI ”Nilikaa MIEZI 8 Bila KUCHEZA”

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad