Spika Ndugai na Cecil Mwambe washtakiwa Mahakama Kuu ya Tanzania



Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania amefungua kesi ya kikatiba dhidi ya Spika wa Bunge Job Ndugai (MB) na aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Ndanda kwa tiketi ya CHADEMA, Cecil Mwambe pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika kesi hiyo ya kikatiba namba 10 ya mwaka 2020, Wakili Paul Kaunda anaiomba mahakama kuu kutengua amri ya spika ya kumtambua Mwambe kama mbunge halali, ilhali mbunge huyo (Mwambe) aliushautangazia umma kwamba amejivua uanachama wa CHADEMA na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Kaunda amesema, kitendo cha spika kumtambua Mwambe kama mbunge halali wakati ameshajivua uanachama wa chama kilichomdhamini ni ukiukwaji wa ibara ya 71(1)(f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977, na hakuna mamlaka yoyote nchini, yenye uwezo wa kumrudisha bungeni mbunge ambaye kwa hiari yake mwenyewe ameamua kujivua uanachama wa chama cha siasa kilichomdhamini kupata ubunge.

Kesi hiyo ya kikatiba imepangwa kusikilizwa Mei 21, 2020 na jopo la majaji watatu litakaloongozwa na Jaji Issa Maige. Majaji wengine ni Stephen Kirimi Magoiga na Seif Kulita.

Katika kesi hiyo, atawakilishwa na jopo la mawakili sita litakaloongozwa na Wakili Mwandamizi Mpale Mpoki akisaidiwa na mawakili Daimu Halfani, Fulgence Massawe, Prisca Chogero, Stephen Msechu pamoja na Stephen Ally Mwakibolwa. 
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad